Binti mateka aliyezama kwenye penzi la mwanamgambo wa Boko Haramu

13Feb 2016
ABUJA, NIGERIA
Nipashe
Binti mateka aliyezama kwenye penzi la mwanamgambo wa Boko Haramu

TAKRIBAN mwaka mmoja baada ya kuokolewa na jeshi la Nigeria kutoka mikononi mwa Boko Haram, Zara John, mwenye umri wa miaka 16, bado amezama kwenye penzi zito na mmoja wa wanamgambo wa kundi hilo la Kiislamu waliomteka.

Wanamgambo wa kundi la Boko Haram

Binti huyo alifurahia kugundua kwamba alikuwa na ujauzito wa mwanamgambo huyo kufuatia vipimo vya mkojo na damu vilivyofanywa na daktari mmoja kwenye kambi ya wakimbizi ambayo alipelekwa baada ya kuokolewa kwake.

"Nilitaka kujifungua mwanangu ili niweze kuwa na mtu wa kuchukua nafasi ya baba yake kwa vile siwezi kuungana naye tena," alisema Zara, mmoja kati ya mamia ya wasichana waliotekwa na wanamgambo wa Boko Haram kwenye uasi wao uliodumu kwa miaka saba sasa kaskazini mashariki ya Nigeria.

Lakini uamuzi wowote juu ya mtoto huyo ulikuwa umeondolewa nje ya uwezo wake.

Baba yake alikufa maji wakati wa mafuriko mwaka 2010 kwa hiyo wajomba zake waliingilia kati kumlea.

Baadhi walikuwa wamegoma wakiwa hawataki uzawa wa Boko Haram kwenye familia yao na kusisitizia kutolewa kwa mimba hiyo. Wengine walihisi mtoto huyo alikuwa hapaswi kulaumiwa kwa uhalifu wa baba yake.

Hatimaye, walio wengi walishinda na Zara aliruhusiwa kubaki na mwanawe, mtoto wa kiume aliyempatia jina la Usman ambaye hivi sasa ana umri wa karibu miezi saba.

"Kila mmoja kwenye familia alimkubali mtoto huyo ," Zara aliueleza Wakfu wa Thomson Reuters kwenye mahojiano ya simu, akiomba kwamba sehemu alipo ibakie kuwa siri.

"Mjomba wangu alimnunulia makopo ya Cerelac na maziwa."
Zara alikuwa na umri wa miaka 14 wakati wanamgambo wa Boko Haram wanaopigana kuanzisha taifa la Kiislamu walipovamia kijiji chake cha Izge, kaskazini mashariki ya Nigeria, Februari 2014.

Walichoma moto kijiji hicho, wakawachinja wanaume, na kuwachukua wanawake, wasichana na watoto na kuondoka nao kwa malori.

Wawili kati ya ndugu wa kiume wa Zara walikuwa nje ya mji wakati wanamgambo hao waliposhambulia kwenye moja kati ya mashambulizi yao ya kuvamia na kukimbia kwenye vijiji pamoja na mabomu ya kujilipua kwenye sehemu za kuabudia na masoko.

Mama yake Zara alianguka kutoka kwenye moja kati ya malori hayo yaliyokuwa yamejaa kupita uwezo wake lakini alijaribu kulifukuzia gari hilo ambalo lilikuwa linaondoka na binti yake huyo wa pekee na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mine, lakini hakuweza kulipata wakati likiendelea na safari ya barabara ya kilomita 22 kwenda Bita.
KUFANYWA WATUMWA NA WANAMGAMBO

Wakati huo, Bita na miji mingine jirani karibu na msitu wa Sambisa, ilikuwa chini ya udhibiti wa Boko Haram.
"Mara tu tulipowasili, walituambia kwamba kuanzia wakati huo tulikuwa ni watumwa wao," Zara alikumbushia.

Siku zake alikuwa akizitumia akifanya kazi za nyumbani na kujifunza imani za dini yake mpya, Uislamu, hadi miezi mwili baadaye, alipotolewa kwa kuolewa na Ali, kamanda wa Boko Haram, na kuhama kutoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na wenzake na kwenda kuishi kwake.

"Baada ya kuwa mke wa kamanda, nilikuwa na uhuru. Nililala muda wowote niliotaka, na niliamka muda wowote niliotaka," alisema binti huyo.

"Alininunulia chakula na nguo na kunipatia kila kitu ambacho mwaname anakihitaji kutoka kwa mwanaume," alisema, akiongeza kwamba vile vile alimpatia simu ya kiganjani huku ikiwa imeandikwa namba yake na mchoro wa jina la Ali kwenye tumbo lake kuonyesha kwamba yeye ni mke wa Boko Haram.

Ali alimhakikishia kwamba mapigano hayo hayatachukua muda mrefu kumalizika na watarudi kwenye mji wa nyumbani kwao wa Baga ambako alikuwa anakusudia mkewe mpya aungane naye kwenye shughuli yake ya uvuvi.

Alimwambia kwamba alikuwa ameachana na biashara yake ya uvuvi na kujiunga na kundi hilo la wanamgambo baada ya baba yake na kaka yake, wote wavuvi kama yeye mwenyewe, kuuliwa na wanajeshi wa Nigeria.

Kwenye ripoti moja ya Juni 2015 ikizungumzia miaka kadhaa ya utafiti na uchambuzi wa ushahidi, shirika la haki za binadamu la Amnesty International lilisema jeshi la Nigeria lilikuwa na hatia ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji makubwa ya raia kwenye sehemu za kaskazini mashariki ya Nigeria, ikitoa wito wa kufanywa uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuwepo uhalifu wa kivita.

Ali hakuwepo nyumbani wakati jeshi la Nigeria lilipovamia Bita mnamo Machi 2015 na kumuokoa Zara na wanawake wengine kadhaa, na kuwachukua kuwapeleka kwenye kambi moja ya wakimbizi huko Yola, kaskazini mashariki ya Nigeria.

Uvamizi huo ulikuja huku ufuatiliaji wa kimataifa juu ya Nigeria ukiongezeka baada ya tukio lililotikisa la utekwaji wa wanafunzi wa kike 200 kutoka Chibok kusini ya Nigeria mnamo Aprili 2014 ambalo lilisababisha hasira kimataifa na kuchochea kampeni duniani ya #bringbackourgirls. Wasichana hao bado hawajapatikana.

Lakini Zara na Ali waliendelea kuwasiliana kwa simu hadi pale wanajeshi wa Nigeria walipokuja kugundua kwamba baadhi ya wasichana hao walikuwa bado wanawasiliana na watu hao waliowateka, wakachukua simu zao na kuwahamishia kwenye kambi nyingine hadi walipounganishwa na familia zao.

Hivi sasa Zara anaishi na familia yake kubwa na mwanawe kwenye mji mmoja mbali kutoka Izge.

Nyumbani na familia yake, ndugu wa kiume wa Zara waliendelea na jukumu la udhibiti wa maisha yake tena, huku maombi ya mahojiano yakiwasilishwa kwao na mienendo yake yote ikifuatiliwa na familia yake.

Lakini alipoulizwa maoni yake, binti huyo alisema ingekuwa bora zaidi kama angekuwa na mumewe huyo wa Boko Haram.

"Kama ningekuwa na njia, ningerudisha namba ya simu ambayo alinipatia," binti huyo alisema, huku akijutia kutokuwa na namba yake kwenye kumbukumbu zake.

Lakini Zara ni mtu anayejua ukweli na anajua kwamba uwezekano wa kuungana tena na Ali ni mdogo sana.

Badala yake anataka kurudi shuleni wakati Usman atakapoacha kunyonya na pengine kuendesha shughuli yake mwenyewe.
"Nataka kufanya biashara ambayo inamfaa mwanamke, kitu ambacho hakitanifanye nitoke nje ya nyumba," alisema.