Undani wa pilika na thamani ya bima ya afya inaangukia katika simulizi ya maisha ya Mama Petra Kajula, mama wa nyumbani na mzazi aliyejifungua hivi karibuni. Anasema, akiwa mjamzito mwaka jana, daktari wake alimwambia angejifungua kwa njia ya upasuaji, hivyo anapaswa kujiandaa kifedha, kukabili haja hiyo.
Petra baada ya kupewa taarifa hizo, anasema zilimchanganya sana, hasa ikizingatiwa ukubwa wa gharama za kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Mama huyo anayemtambulisha mume wake ni dereva wa bodaboda na uchumi wao uko chini, anasimulia taarifa hizo na daktari zilimpa wakati mgumu, akiwaza moja kwa moja uwezekano wa wao kumudu gharama za upasuaji ulivyo mdogo.
Akafafanua kipato chao, kilitosha kulipia gharama zao za maisha za kila siku pekee.
Petra anaeleza kwamba mwezi aliotarajia kujifungua ulikuwa umekaribia na wakati anapata taarifa hizo, familia yake ilikuwa imejiandikisha katika Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (CHF), tangu mwaka 2021, lakini walikuwa bado hawajalipia.
Uamuzi waliofikia na mumewe, wakapambana na kufanikiwa kulipia, huku akikiri kwamba, kabla ya kujiandikisha walikuwa hawaoni umuhimu wa kujiandikisha kwenye bima hiyo, ila picha kamili ya thamani ya bima, ikajionyesha penye hitaji la kiafya lilipochukua nafasi.
“Kwa hiyo ni muhimu sana watu kujiandikisha na kupatiwa bima ya afya kwa sababu inasaidia kupunguza gharama tofauti na ambavyo ukikumbwa na magonjwa, unatumia fedha nyingi kama hakuna msaada wa bima,” anasimulia Petra. Anaendelea: “Nimekuwa shuhuda wa hili na nashukuru imenirahisishia katika hatua yangu ya kujifungua ambayo ilikuwa ni kwa upasuaji.”
MRATIBU CHF Bernard Shaba, Mratibu wa Bima ya ‘CHF’ katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, anakoishi Petra, anasema awali hapakuwapo mwitikio wa kutosha wa wananchi kujiunga na bima ya afya, hasa kutokana na kukosekana taarifa za kutosha kuhusu umuhimu wa bima.
Anasema tayari wameanza kufanya jitihada za kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa njia mbalimbali, ikiwamo kupitia vipindi vya redio za jamii.
“Watu wachache sana walikuwa wanajiunga bima ya afya kwa sababu hapakuwa na taarifa za kutosha, lakini baada ya vipindi vya redio, watu wengi sasa wameanza kufahamu jambo hili.
“Hata tunavyozungumza, ongezeko la watu wanaoomba kujiunga bima kwa sasa ni kubwa, lakini pamoja na mwitikio huo tunaouona, tutaendelea kutoa elimu zaidi,” anasema.
NGUVU YA UWEZESHAJI Ni mradi unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), zikiwezesha mamlaka za serikali toka wilayani Rungwe, mkoa wa Mbeya, anasema: “Elimu kuhusu bima hii, niliisikia kwenye redio ya hapa kwetu. Kabla ya hapo nilikuwa nauza hadi mifugo yangu ikiwamo ng`ombe ili nipate fedha ya kunisaidia kwenye matibabu na wakati mwingine unafilisika, unabaki masikini kwa ajili ya kuuza vitu kugharimia matibabu hayo.”
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii (TAMISEMI), Dk. Ntuli Kapologwe, anasema asilimia 86 ya wananchi hawajajiunga na bima ya afya nchini, kutokana na kukosa elimu sahihi ya umuhimu wake.
Anasema, kwa sasa serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2022, ikiwa katika hatua ya subira ya bunge kupitisha muswada kuwa sheria.
Mnamo Novemba mwaka jana, Bunge lilirejesha muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote mwaka 2022 kwa Kamati ya huduma za Maendeleo ya Jamii kwa mashauriano zaidi.
Kupitia Sheria inayopendekezwa, inatarajiwa kuruhusu kuwapo kwa skimu binafsi za Bima ya Afya ambazo zitatoa huduma za Bima ya Afya kwa wananchi katika sekta rasmi binafsi na isiyo rasmi.
Pia, inampa nafasi waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya, kupitia kanuni na kuweka viwango vya uchangiaji kwa kuzingatia uhitaji wa huduma, gharama halisi za matibabu na uwezo wa wananchi kuchangia. Kadhalika, kuna wasio na uwezo watakuwa na haki ya kupata huduma za matibabu kupitia utaratibu utakaowekwa na serikali baada ya kuwatambua kupitia mfumo maalumu wa utambuzi utakaowekwa.










