2022 mwaka usio na matukio makubwa Tanzania

28Dec 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SAALAM
Nipashe
2022 mwaka usio na matukio makubwa Tanzania
  • Ni mwendokasi wa maendeleo, kutegeana kisiasa

MWAKA unaomalizika wa 2022 ulikuwa wenye kila la kufurahisha hapa nchini ukilinganisha na yaliyokuwa yanaendelea katika mataifa mengine. Ahueni ya mwaka huu inatokana na ukweli kuwa 2021 na hata 2020 ulikuwa na unafuu na kupungua kwa UVIKO -19.

Rais Samia Suluhu Hassan, akishuhudia Bwawa la Mwalimu Nyerere moja ya miradi mikubwa ya kimkakati, likijazwa maji hivi karibuni. PICHA: MAKTABA

Pengine siyo kwamba watu hawakufariki kwa maradhi hayo lakini huwezi kulinganisha na idadi ya waliopoteza maisha kwingineko duniani.

Kwa suala hilo kuna jambo la kuongeza tafakari kuwa kwenye mwisho wa mwaka huu wakati dunia kwa jumla inaanza kuusahau UVIKO-19, nchini China sasa unapamba moto.

Tatizo limeendelea kuwapo hata baada ya kukwama kwa sera ya 'zero COVID,' inayohusisha kufungia watu ndani na kutoa vibali maalum baada ya kupima ili kudhibiti maradhi hayo.

MIRADI KIMIKAKATI

Mwaka 2022 Watanzania wanashuhudia ukamilishwaji na mwendelezo wa miradi na mikakati iliyoanzishwa wakati wa awamu ya tano ambako Rais Samia Suluhu Hassan, aliahidi kila ambacho serikali ilikianzisha hakitaachwa na awamu ya sita.

Kuanzia 2021 na hata 2022 zilitafutwa nyenzo nyingine kwa mfano tozo katika kupelekeana fedha kwa njia ya simu, ingawa viwango vilivuka mpaka katika bajeti ya 2022 ikabidi virekebishwe visilete madhara kibenki na kisera.

Kwa jumla jitihada zilizobaki za kujenga miundombinu, reli ya kisasa SGR, kukamilisha bwawa la umeme la Julius Nyerere ambalo sasa limeanza kujazwa maji, viko pia vituo vya afya na shule mpya pamoja na madarasa mengi zaidi yanajengwa kwa kasi.

Yako maeneo ambayo kasi inashangaza, kwa mfano kukamilisha kufikisha umeme vijiji vyote hadi kufikia mwisho 2025.

Eneo ambalo kwa upande fulani lilikuwa na mwendo halisi wa kutatua matatizo halafu mikwamo ya wazi inayotokana na baadhi ya maelekezo ya awamu ya tano, ni mdahalo kuhusu mfumo wa siasa na hasa kuvizuia vyama vya siasa kuendesha shughuli zake kwa mwaka wa saba sasa.

Ni suala ambalo serikali imesikika ikiahidi kuwa  inakaribia kutoa rasimu ya kukubali mapendekezo ya kikosi kazi cha kuboresha demokrasia, hasa suala la mikutano ya hadhara ya vyama inayoruhusiwa kikatiba ndilo eneo nyeti zaidi.

kwa ujumla jambo hilo, mwaka 2022 ulianza kwa kiongozi wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu kukutwa na mahakama kuwa wana kesi ya kujibu, ambayo bila shaka ingechukua muda mrefu na kuendelea kudumaza shughuli za siasa, kujenga uhasama zaidi, hadi kufikia 2025 wakati wa uchaguzi mkuu, hiyo ilikuwa Februari 2022 .

Mwezi Machi mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka Sylvester Mwakitalu, akatangaza kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo na kwa maana hiyo Mbowe akaachiwa huru.

Ni katika kufikia maridhiano na uhimilivu wa kisiasa Mbowe anafika Ikulu akiteta na Rais Samia, kukawa na matumaini ya maelewano.

Suala la wabunge 19 wa viti maalum waliofukuzwa  CHADEMA, baada ya Mbowe kuteta na Rais Samia, mwenyekiti huyo aliashiria katika hotuba Iringa aliposhirika hafla ya Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) kuwa ingefaa suala hilo liachwe. Ingekuwa ni hatua ya kwanza ya maelewano ila ikakwama Baraza Kuu, jambo likaachwa pembeni na sasa kesi inaendelea mahakamani ukibaki kuwa mkwamo unaodumu.

Baada ya mkwamo huo wa vielelezo vya maelewano mkakati wenyewe wa maelewano ukabakia, kikaundwa Kikosi Kazi cha kuweka sawa mfumo wa kidemokrasia wa kuendesha vyama vya siasa. Inawezekana kweli zipo kanuni zitarekebishwa lakini kama ilivyo katika urekebishaji wa sheria ya vyombo vya habari, si rahisi kutazamia kuwa serikali ijivue uwezo wa kuingilia kati, kuonya, kudhibiti au kuzuia.

Ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki 2022 ni mwaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilipojiunga na Jumuiya, kuwezesha suala la amani mashariki ya nchi hiyo liwe la kikanda.

Nchi kadhaa zinataka kufanya biashara halali na DRC ambayo inasimamiwa na mifumo kama umoja wa forodha, hati ya kusafiria ya kijumuiya, soko la pamoja na sasa Soko Huria la Afrika ambalo limeridhiwa kwa viwango tofauti.

Kuendelea kwa vikosi vya waasi kudhibiti eneo hilo na kuchota madini huku haki za binadamu zinavunjwa ni mkakati ambao muda wake umepita. Licha ya M23 kujizatiti kwa mapambano kikamilifu sambamba na juhudi za kupata amani zinazoendelea Nairobi na Angola.

Eneo jingine ambako limeonekana mbele ya dunia nzima ni jinsi Rais Samia alivyomudu kuteka hisia za watu na kuonyesha mbinu mbadala za maendeleo, nje ya kuendeleza miradi mikubwa.

Amefikisha uwezekano wa makubaliano kwa miradi kama Bandari ya Bagamoyo kuanza tena kutangaza zabuni za ujenzi wake, mradi wa kuchakata gesi asilia mkoani Lindi ambao kimsingi una uwezekano wa kubadili sura ya nchi kimapato na kukamilisha itifaki ya kuanza kuchimba njia ya bomba la mafuta kutoka kaskazini ya Uganda kwenda Tanga.

Bomba la mafuta kwenda Zambia sasa linapata kasi mpya ya kusafirisha gesi kutoka Dar es Saalam, halafu kuna bomba la gesi kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa limeshaafikiwa. Ni diplomasia ya uchumi ya kasi na mageuzi.

Tukio ambalo lilimpambanua Rais Samia heshima kwa haiba yake na kujituma ni kushiriki filamu ya 'Tanzania: The Royal Tour' Inaelekea kuwa ilifaulu kuchochea utalii, pamoja na hatua nyingine za diplomasia ya uchumi zilizofanya Tanzania ing'are katika mageuzi ya uchumi mwaka uliopita.

Rais Samia anakuwa kiongozi mkuu wa kwanza kutoka nje aliyekaribishwa China baada ya mkutano mkuu wa Chama cha Kikomunisti kilichomthibitisha Rais Xi Jinping katika nafasi hiyo akiitumikia nchi yake kama kiongozi wa maisha.

Alipoingia madarakani mwaka 2013 Tanzania ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza kuitembelea nje, kama ambavyo Rais Barack Obama alipoingai madarakani mapema 2009 kiongozi wa kwanza kutoka Afrika aliyepewa nafasi ya kumwona Ikulu ya Washington alikuwa Rais Jakaya Kikwete, hivyo Rais Samia anajenga katika misingi iliyokuwa imara.