Wachezaji wengi, hasa kwenye klabu za Simba, Yanga na Azam FC, na wachache kutoka timu zingine za mikoani, walisajili wachezaji kutoka pande mbalimbali za Afrika ili kutia chachu na kuwapa changamoto wachezaji wazawa.
Baadhi ya wachezaji wamethibitisha kuwa wao ni wa 'kimataifa' na kuzitendea vyema klabu ambazo zilitumia fedha kuwagharamia kutoka katika timu walizotoka na kuwaleta nchini.
Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya wachezaji kutoka nje ya nchi wakiongozwa na Abdolauye Pape Ndaw wa Simba, waliwashangaza mashabiki wengi wa soka kutokana na viwango vyao vya hali ya chini ukilinganisha hata na wachezaji wa Kibongo.
Mwandishi wa makala haya kwa mujibu wake, ameorodhesha kikosi bora kabisa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2015/16.
Hawa ni 'mapro' walioonyesha kuwa wanastahili kulipwa mishahara minono, kwa kuonyesha viwango endelevu na vya hali ya juu.
1. Vicent Angban-Simba
Nadhani kama si umakini wake, Simba isingekuwa hata kwenye nafasi hii iliyopo.
Ni mmoja wa makipa bora kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Nadhani kama kipa huyu kutoka nchini Ivory Coast atapata mabeki bora, kila mmoja anaweza kuthibitisha hili.
Alitatizwa kidogo kupwaya kwa mabeki wa timu yake. Lakini jinsi anavyosimama golini, kupanga mabeki, kujiamini, kucheza mipira ya krosi, kutumia vyema urefu wake, lakini pia kuweza kuwatuliza mabeki wake wanapochanganyikiwa ni mambo yanayompa sifa ya kuwa kipa bora.
Viongozi wa Simba wamekaririwa kukoshwa na uwezo wake na kutaka kumpa mkataba mpya.
2. Mbuyu Twite-Yanga
Ni beki mzoefu kwenye soka la ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Raia huyu wa Rwanda mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) anacheza kwa kutumia nguvu, akiwa pia na uwezo wa kucheza karibuni namba zote za nyuma, pamoja na kiungo mkabaji.
Sifa yake nyingine ni uwezo wa kurusha mpira kwa umbali mrefu. Naye ameorodheshwa kwenye kikosi hiki kwa sababu ameendelea kufanya vizuri.
3. Pascal Serge Wawa-Azam FC
Hakuna ubishi kuwa ni mmoja wa mabeki bora kabisa kwenye Ligi Kuu.
Mashabiki wa soka wamempachika majina mengi sana kama 'Mguu wa chuma', 'Kaka mkuu' na mengine mengi.
Raia huyo wa Ivory Coast ni mmoja wa mabeki wachache nchini waliojaliwa nguvu, akili na pia uwezo wa kumiliki mpira, kitu ambacho ni nadra sana kwa mabeki wa Kitanzania kuwa navyo vyote. Kutokana na uwezo wake huo, anaweza kabisa kucheza beki tatu.
4. Vicent Bossou-Yanga
Ni beki ambaye mwanzo alionekana kuwa ni garasa. Ghafla ameibuka kuwa ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Yanga.
Bossou, ambaye ni raia wa Togo ana umbile halisi la u-beki. Ni mrefu na ana nguvu, hivyo kuweza kukabiliana kwa namna yoyote ile na washambuliaji wasumbufu na wenye nguvu.
Ingawa hana kasi, lakini mapungufu hayo kuyaziba kwa kuhakikisha kuwa hamruhusu straika kumpita kirahisi.
5. Juuko Murshid-Simba
Pata picha kama beki huyu wa Simba atacheza timu moja na Bossou.
Staili yake ya kukaba ni ile ya kutomruhusu straika kupita kwa njia yoyote ile.
Ni mmoja wa mabeki wakorofi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, mwenye rafu za kisiri, zisizoonwa na waamuzi wengi.
Hata hivyo, amekuwa ni mhilimili mkubwa kwenye kikosi cha Simba na angalau ndiye anayehofiwa na mastraika wa timu pinzani.
Mganda huyu anastahili kucheza 'mkoba' kwenye kikosi hiki, akimaliza nyumba ya Bossou.
6. Youssuof Sabo-Coastal
Pamoja na kushuka daraja, Coastal ilikuwa imempata mmoja wa viungo bora kabisa kutoka nchini Cameroon Youssof Sabo.
Katika mechi ambazo timu hiyo ilicheza dhidi ya Simba, Yanga na Azam, kijana huyo aliwafunika viungo wa timu zote hizo.
Mbali na hilo, ni uwezo wake wa kupachika mabao, tofauti na viungo wengi wakabaji wa Kibongo ambao ni aghalabu sana kuwa na sifa hiyo.
Uwezo huo alikuwa nao marehemu Patrick Mafisango. Ndiyo maana kijana huyo amechukua nafasi hii hapa na si Justice Majabvi.
7. Kipre Tchetche-Azam
Sina haja sana ya kumuelezea winga huyu ambaye wakati mwingine anachezeshwa kama mshambuliaji.
Ana misimu kadhaa akicheza soka la Tanzania. Raia huyu wa Ivory Coast ndiye kwa sasa ni mmoja wa wachezaji nembo kwenye kikosi cha Azam FC.
Anapewa namba saba kwenye kikosi hiki kama kawaida yake.
8. Thabani Kamusoko-Yanga
Unataka nini tena kwenye kikosi chako kama una kiungo mshambuaji kama huyu.
Kamusoko, raia za Zimbabwe, amejitofautisha na viungo wengi nchini wanaocheza kwa mbwembwe nyingi na kushangiliwa majukwaani kwa kupiga pasi nyingi zisizo na madhara.
Hana mambo mengi, anapokea mpira na kupiga pasi ambazo mara nyingi ni za hatari.
Pia, ana uwezo wa kuamua kupasua mwenyewe iwapo ataona mastraika wake wamebanwa.
Ni kiungo mwenye uwezo wa kupachika mabao, akiwa na magoli matano kwenye Ligi Kuu.
9. Donald Ngoma-Yanga
Huyu ndiye mshambuliaji. Kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara wamekosekana washambuliaji wenye nguvu na purukushani tangu walipoondoka kina Joseph Kaniki 'Golota'.
Amepatikana Ngoma, mwenye kasi, nguvu na uwezo wa kucheza soka la aina yoyote ile.
Raia huyu wa Zimbabwe amekuwa mfano kwa washambuliaji wengine chipukizi jinsi mchezaji wa eneo hilo anavyopaswa kuwa.
10. Amissi Tambwe-Yanga
Kama unataka magoli, bali huyu ndiye straika anaweza kukupatia goli dakika yoyote ile.
Ni kwamba anapokuwa uwanjani, shabiki unatarajia kuwa kosa moja la beki linaweza kusababisha afunge goli.
Ni lazima apate namba kwenye kikosi chochote kile kama timu inacheza kwa kutafuta ushindi na si kujilinda.
Raia huyu wa Burundi anaongoza kwenye orodha ya wafungaji bora msimu huu kwa mabao 21 aliyonayo.
Kwake yeye kupiga 'hat-trick', au kuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ufungaji bora si tatizo kubwa.
11. Hamisi Kiiza-Simba
Mfumo wa uchezaji kwenye kikosi hiki ni 4-3-3. Ina maana washambuliaji ni watatu. Ndiyo maana mshambuliaji wa Simba Hamisi Kiiza amewekwa namba 11. Ni kwamba atakuwa anasaidiana na Ngoma na Tambwe.
Kama Tambwe, ni aina ya washambuliaji wanaoweza kukuadhibu kwa kosa moja ambalo unaweza kulifanya.
Raia huyu wa Uganda, amekuwa ndiye kinara wa upachikaji mabao kwa upande wa Simba, lakini akichuana vikali na Tambwe kuwania kiatu cha dhahabu.
Wachezaji wa akiba
Hanington Kalyesubula (Uganda)- Mbeya City
Issoufou Boubacar (Niger)-Yanga
Haruna Niyonzima (Rwanda)-Yanga
Justice Majabvi (Zimbabwe)- Simba
Michael Ballou (Ivory Coast)- Azam
Didier Kavumbagu (Burundi)- Azam
----------------------------------










