‘Big Six’ za EPL ilizofanya usajili bora msimu 2023-24

08Aug 2023
Na Mwandishi Wetu
UINGEREZA
Nipashe
‘Big Six’ za EPL ilizofanya usajili bora msimu 2023-24

MSIMU wa Ligi Kuu England wa 2023-24 unaoanza Ijumaa hii kwa maana zimebakiza siku tatu tu kabla ya kuanza. Mabingwa Watetezi wa ligi hiyo, Manchester City, watacheza na Burnley iliyopanda daraja, Agosti 11, mwaka huu ili kuanza kampeni mpya.

 

 

Kwa wiki kadhaa zilizopita, klabu zimekuwa zikijiandaa kwa ajili ya msimu mpya kwa kushiriki katika mechi za kirafiki za kabla ya msimu mpya na pia zikifanya makubwa kwenye soko la uhamisho wa wachezaji majira haya ya joto.

Dirisha la usajili ni wakati muhimu kwa klabu sita kubwa 'Big Six' kwani ubora wa mikataba wanayofanya katika kipindi hiki inaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yao msimu huu. Zaidi ya hayo, kuambatana na wapinzani wengine kati ya sita bora kunamaanisha kila klabu lazima iandae kikosi chenye uwezo kwa ajili ya msimu.

Kwa klabu za Ligi Kuu England, dirisha la uhamisho wa wachezaji halijafungwa hadi Septemba Mosi, mwaka huu. Hata hivyo, wakati msimu mpya ukiwadia, makala haya yanaangalia kwa kina jinsi klabu hizo za 'Big Six' zilivyofanya hadi sasa kwenye soko la uhamishaji linaloendelea.

Bila kuchelewa zaidi, tunazitazama klabu sita kubwa za Ligi Kuu England kulingana na aina ya wachezaji waliosajili hadi sasa...

 

#6 Manchester City

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City ndio imekuwa klabu iliyosajili wachezaji wachache kati ya klabu kubwa sita bora msimu huu wa majira ya joto hadi sasa. Hakuna jambo la kushangaza kwani Pep Guardiola bado ana kiini cha kikosi chake kilichoshinda mataji matatu msimu uliopita.

Hadi sasa Man City wamekamilisha dili moja pekee. Mateo Kovacic alijiunga na mabingwa hao mara sita wa Ligi Kuu kutoka Chelsea kwa kitita cha pauni milioni 25, akichukua nafasi ya Ikay Gudogan aliyehamia Barcelona kwa uhamisho wa huru.

Hata hivyo, City imekuwa ikihusishwa na kutaka kumsajili Josko Gvardiol na wanapewa nafasi kubwa ya kumnasa beki huyo wa Croatia. Kwa mujibu wa mwandishi wa habari za usajili, Fabrizio Romano, klabu hiyo imefikia makubaliano binafsi na mchezaji huyo, lakini bado haijakamilisha makubaliano na RB Leipzig.

Pia kuna uwezekano mkubwa kwamba City wanaweza kufanya usajili wa ziada kabla ya dirisha kufungwa. Riyad Mahrez alijiunga na Al-Ahli hivi majuzi, na kuna uwezekano kwamba klabu hiyo inaweza kuwa inatafuta mchezaji mpya wa kuziba pengo la Mualgeria huyo.

 

#5 Tottenham Hotspur

Tottenham imefanya kazi kubwa msimu huu wa majira ya joto. Wamemleta kocha mpya na kuongeza majina mapya kwenye orodha ya kikosi chao. Kocha wa zamani wa Celtic, Ange Postecoglou ataiongoza klabu hiyo katika msimu mpya.

Spurs wamemsajili kiungo wa kati wa England, James Maddison kutoka Leicester City iliyoshuka daraja kwa pauni milioni 40. Pia wamemsajili Guglielmo Vicario kutoka Empoli kwa pauni milioni 17.

Mshambuliaji huyo wa Italia atachukua nafasi ya Hugo Lloris ambaye anasaka klabu mpya baada ya kuachwa kwenye kikosi cha maandalizi ya msimu mpya.

Mshambuliaji wa Israel, Manor Solomon pia alijiunga na klabu hiyo ya Kaskazini mwa London kwa uhamisho wa huru kutoka Shakhtar Donetsk. Mikataba ya mkopo ya Pedro Porro na Dejan Kulusevski imefanywa kuwa ya kudumu pia.

 

#4 Chelsea

Chelsea imekuwa klabu yenye shughuli nyingi zaidi kati ya timu kubwa sita katika masuala ya uhamisho wa jumla katika dirisha la sasa. Marekebisho makubwa katika Uwanja wa Stamford Bridge yamewafanya wachezaji 10 wa kikosi cha kwanza kuondoka msimu huu.

Mason Mount, Mateo Kovacic na Kai Havertz wamejiunga na wapinzani wao wa Ligi Kuu Manchester United, Manchester City na Arsenal. Edouard Mendy na Kalidou Koulibaly, wamehamia Saudi Arabia huku N'Golo Kante na Cesar Azpilicutea pia wakiondoka kwa uhamisho huru. Wachezaji wengine ambao wameondoka 'Blues' ni pamoja na Pierre Emerick Aubameyang, Christain Pulisic na Ruben Loftus-Cheek.

Kumekuwa na wachezaji wawili wakuu waliowasili katika klabu hiyo hadi sasa. Christopher Nkunku (pauni milioni 52) na Nicolas Jackson (pauni milioni 32) walinaswa kutoka kwa RB Leipzig na Villareal ili kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Vijana Angelo Gabriel na Diego Moreira pia wamenaswa na klabu hiyo. Angelo, Mbrazil amejiunga kutoka Santos, wakati Moreira mwenye umri wa miaka 18, ametua kwa uhamisho huru kutoka Benfica.

 

#3 Liverpool

Baada ya kampeni mbaya ya 2022-23, ilionekana wazi kuwa Liverpool ilihitaji vipaji vipya katika klabu hiyo. Hasa katika idara ya kiungo ambapo waliteseka sana kutokana na majeraha kwa baadhi ya wachezaji wao muhimu.

Ili kuchukua wachezaji wapya, ilikuwa ni lazima kuwaondoa wale ambao hawakuwa wakicheza kwa viwango. Naby Keita, James Milner, Roberto Firmino, na Alex Oxlade-Chamberlain wote wameondoka kama wachezaji huru.

Kuziba pengo la kiungo, 'Wekundu' hao wametumia pauni milioni 95 kuwanunua Dominik Szoboszlai na Alexis MacAllister kutoka RB Leipzig na Brighton & Hove Albion.

Usajili zaidi unatarajiwa kutoka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu wa mwaka 2020 ambao walimpoteza Jordan Henderson hivi karibuni kwa Al-Ettifaq. Fabinho pia amejiunga na Al-Ittihad.

 

#2 Manchester United

Manchester United wana wachezaji wawili wakubwa waliosajiliwa hadi sasa. Mason Mount kutoka Chelsea (pauni milioni 60), na Andre Onana kutoka Inter Milan ambaye amechukua nafasi ya David De Gea aliyeondoka. Beki wa zamani Johnny Evans pia alisaini mkataba wa muda mfupi wa kujiandaa na msimu mpya na klabu hiyo.

'Mashetani Wekundu' hao pia wamekubali dili la kumsajili fowadi wa Atlanta, Rasmus Hojlund. Kama ilivyoripotiwa kupitia gazeti la The Mirror, mchezaji huyo wa Kimataifa wa Denmark ataigharimu timu hiyo pauni milioni 72.

 

#1 Arsenal

Baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, ilidhihirika wazi kwamba klabu hiyo ya London inahitaji moto zaidi ili kuweza kuchuana na timu nyingine kubwa, hasa Manchester City.

Arsenal kwa kiasi kikubwa imekuwa ikifanya kazi zaidi katika soko la usajili linaloendelea katika ‘Big Six’. Hii ni kwa sababu 'Washikabunduki' hao wametumia fedha nyingi zaidi kwa uhamisho unaoingia hadi sasa.

Kwa mujibu wa soko la uhamisho, timu hiyo ya Mikel Arteta imetumia euro milioni 231.60 kupata wachezaji watatu tu msimu huu wa majira ya joto. Declan Rice alichukuliwa kutoka West Ham United kwa ada ya rekodi ya klabu ya pauni milioni 105. Kai Havertz na Jurrien Timber pia wamejiunga na Washikabunduki hao kutoka Chelsea na Ajax.