Kiongozi huyo pia amekubali mpango wa kikanda wa mpito unaoweka mazingira kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati.
Nchi za Karibiani zimefanikisha mpango huo wa Ariel Henry kujiuzulu wakati wa mkutano wa dharura huko Jamaica. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken alitoa dola milioni 100 zaidi kufanikisha usalama ambapo timu ya Jeshi la Kenya inaongoza vikosi vya ulinzi.
Makundi yenye silaha yamechukua sehemu kubwa ya nchi maskini zaidi huko Amerika Kusini na katika wiki za hivi karibuni, mgogoro umezidi kuwa wa ghasia zaidi. mashuhuda wamesema kumekua na ongezeko la maiti kurundikana barabarani, majambazi wenye silaha wakiteka miundombinu muhimu, na pia kuna hofu ya ongezeko la njaa.
"Serikali ninayoiongoza haiwezi kuendelea kuwa kiziwi kwa hali hii. Kama nilivyosema daima, hakuna dhabihu kubwa mno kwa ajili ya nchi yetu ya Haiti," Henry amesema katika hotuba ya kujiuzulu aliyoiweka mtandaoni.
Viongozi wa makundi ya wahalifu walikuwa wamedai kuondoka kwa Henry ambaye, ingawa alijitambulisha kama mtu wa muda, alikuwa madarakani tangu mwaka 2021 wakati Rais wa Haiti alipouawa. Haiti haijafanya uchaguzi tangu mwaka 2016.
Rais wa Guyana Irfaan Ali, ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya kikanda ya CARICOM, ametangaza baada ya mwisho wa wiki ya diplomasia kwamba Henry atajiuzulu mara tu mamlaka mpya ya mpito itakapowekwa.