Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema hayo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra Chiwelesa.
Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji mpango wa serikali katika kunusuru uchumi wa nchi kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni, hususani Dola ya Marekani.
Akijibu swali hilo, Dk. Nchemba alisema pamoja na vikwazo vilivyopo, upatikanaji wa fedha za kigeni nchini ni himilivu na kiasi kilichopo kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.7 ikilinganishwa na malengo ya miezi minne.
Serikali, alisema inaendeleea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi wa kati na muda mrefu katika kukabiliana na vikwazo ya upatikanaji wa fedha za kigeni, hususani Dola ya Marekani.
“Vikwazo hivyo vimesababishwa na athari za vita kati ya Ukraine na Russia, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii baada ya UVIKO-19 na mabadiliko ya tabianchi.
“Sababu nyingine ni utekelezaji wa sera za fedha ambayo inalenga kupunguza ukwasi katika uchumi wa nchi mbalimbali ikiwamo Marekani ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei. Kwa ujumla, matukio hayo yameathiri mnyororo wa uzalalishaji, usambazaji na uhitaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia,” alisema.
Alitaja hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kupunguza athari za upatikanaji huo ni pamoja na kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni. kati ya Machi, 2022 na Agosti, mwaka huu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeuza katika soko la fedha za kigeni zaidi ya dola za Marekani milioni 500.
Pia alisema jitihada zingine ni kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu, kutekeleza mikakati ya kuongeza mauzo nchi za nje na kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Kadhalika, alisema serikali imepanga kuendelea kushirikisha benki za biashara, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni pamoja na wadau wengine katika kusimamia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za kigeni nchini.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji mkakati wa serikali wa kunusuru wakandarasi ambao wameathiriwa na upungufu huo wa Dola na mkakati wa serikali wa kuhakikisha hauathiri utekelezaji wa bajeti.
Akijibu swali hilo, Waziri Nchemba alisema serikali imechukua hatua ya kuhakikisha inabana matumizi ili kutoa fursa miradi ya wananchi isiathiriwe.










