Tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:00 asubuhi katika kitongoji cha Namba Tisa “A” akiwa kwenye shamba lake la miti huku sababu za kutekeleza tukio hilo zikiwa hazijafamika mpaka sasa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Manjala alijipiga risasi chini ya kidevu na sikio la kulia. Alisema chanzo bado hakijafahamika na wameuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi.
Alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi kwa kuwahoji ndugu, jamaa na marafiki ili kubaini chanzo cha tukio hilo na utakapokamilika watakabidhi mwili kwa ndugu ili kuendelea na taratibu za mazishi.
Diwani wa Kata ya Ulowa, Gabriela Kimaro, alisema tukio hilo limewashangaza kutokana na uamuzi aliochukua mkulima huyo maarufu kwa kuwa wamezoea kusikia watu wanajinyonga kwa kamba na kuacha ujumbe mbalimbali lakini amejiua kwa kujipiga risasi bila kuacha ujumbe wowote.
Alisema licha ya kuwa mkulima mkubwa na kuiingizia mapato Halmashauri ya Ushetu, pia alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ulowa.
Kimaro alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo, Manjala aliamka akiwa mzima na alionekana shambani kwake kama mtu anayekagua shamba lake lakini baadaye ulisikika mlio wa risasi na baadaye kubainika kuwa amefariki dunia kwa kujiua.
“Sisi sote hapa hatufahamu sababu iliyomfanya kujipiga risasi shambani kwake tena kwa kujipiga risasi kwenye koo hadi risasi kutokeza kichwani. Tunasubiria taarifa ya Polisi baada ya kumaliza upelelezi, hivyo niwaombe wananchi watulie,” alisema Kimaro.
Diwani wa Nyamilangano, Robert Mihayo, alisema Manjala alikuwa mmoja wa wakulima wanaochangia mapato ya ndani ya halmashauri kutokana na mamlaka hiyo ya serikali za mitaa kutegemea mapato kupitia zao hilo.
Alisema watu wanapopata msongo wa mawazo waache kuchukua sheria mkononi badala yake watafute ushauri kwa watu wa karibu yao.
Mihayo alisema siku kadhaa zilizopita walishiriki naye katika mkutano mkubwa uliofanyika Kata ya Ulewe uliokuwa umeitishwa na Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, na wameshangaa kupata taarifa kuwa amejipiga risasi shambani.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kahama, Hassan Haruna, alisema chama kimepokea msiba huo kwa masikitiko na taarifa za kifo hicho alizipata kwa wanajumuiya walioko Ulowa na sababu za kifo hicho bado hazijafahamika.









