Akizindua harambee ya kuchangia Chama cha Wanaume Wazee Tanzania iliyofanyika jijini Arusha , Waziri Gwajima alisema wazee ambao ni viongozi wa familia wana nafasi kubwa katika maadili ya vijana.
"Katika zama hizi tunahitaji zaidi wazee waendelee kufanya mengi ili kuambukiza vizazi vipya tabia njema na kuwezesha nao kufikia uzee ulio mwema.
"Cha kusikitisha hivi karibuni kumekuwa na baadhi ya wazee wanaoripotiwa kufanya matukio ya ajabu yasiyolingana na umri wao, mfano kubaka na kulawiti watoto, kuwaoza watoto wadogo na kupandikiza imani mbaya," alisema.
Kutokana na mmomonyoko wa maadili kushamiri ndani ya jamii, Waziri Gwajima alisema wazee wanatakiwa kuhakikisha wanawalea vijana kwa ajili ya maisha yao ya uzeeni.
Waziri huyo alisema wazee wana nafasi kubwa ya kukemea vitendo vyovyote ambavyo ni kinyume cha maadili ya jamii ya Kitanzania.
"Kwa sasa tunapita katika kipindi cha mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii, hili ni changamoto na wazee tusiposimama vizuri kwa nafasi yetu kubeba ulezi wa jamii, tutajikuta tunapata wazee wa kesho na keshokutwa ambao watashindwa kulea vizazi vinavyokuja," alionya.
Waziri Gwajima alisema chombo hicho kina ulazima wa kuwa na jukumu la kujua kinafanya nini ili maadili ya vijana yaendelee kuwa mazuri kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Pia alikitaka chama hicho kushirikiana kwa karibu na Baraza la Ushauri la Wazee na serikali katika kutekeleza afua mbalimbali kwa ustawi wa wazee.
Katika uzinduzi huo, kiongozi huyo alieleza juhudi za serikali zinazofanywa kuhakikisha ustawi wa wazee ikiwamo kuimarisha mifumo, ili wazee wapate huduma za kijamii kama afya, ulinzi, usalama na matunzo kwenye makazi ya wazee.
Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Tadey Mchena alisema wanakusudia kupata Sh. milioni 100 kwa lengo la kununua kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya chama, kuelimisha jamii, kuwasaidia wazee bima ya afya na vitendea kazi.
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Sagata alisema wana malengo ya kuwasaidia wazee katika masuala mbalimbali ikiwamo matibabu kupitia bima ya afya.
Katika harambee hiyo zilikusanywa Sh. milioni 30, ahadi ikiwa Sh. milioni 11 na fedha taslimu Sh. milioni 19 huku Waziri Gwajima akichangia Sh. milioni mbili.










