Uteketezaji huo ulifanyika juzi katika Kiwanda cha Chilambo Generation Company Limited kinachojihusisha na uchakataji wa taka kilichoko Kisarawe mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, James Mbalwe alisema mashine zilizoteketezwa ni sehemu ya zilizokamatwa na bodi hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuanzia mwezi Julai hadi Agosti mwaka huu katika mikoa ya Pwani, Lindi, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Manyara na Songwe.
Alisema mashine hizo zilikamatwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kufanya biashara bila leseni, kuingizwa nchini kinyemela, kufanya biashara katika maeneo ambayo hayaruhusiwi na kukwepa kodi.
“Kwa ujumla, mashine hizi zinaitia hasara serikali jumla ya Sh. milioni 33 kwa mwezi, sawa na Sh. milioni 400 (kiwango halisi Sh. milioni 396) kwa mwaka pamoja na kukwepa kodi na tozo mbalimbali kinyume cha sheria.
"Kibaya zaidi waendeshaji haramu wamekuwa wakiwaruhusu watoto kushiriki michezo hiyo, kitu ambacho ni kinyume cha sheria," alifafanua.
Vilevile, alisema katika operesheni hiyo, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanane na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria na mashauri yao yako kwenye uchunguzi.
“Mashine tulizozikamata ni 416, lakini leo (juzi) tumeteketeza mashine 300 kwa sababu hizo 116 zipo nje ya mkoa huu. Hizo nazo tutazileta hapa zitateketezwa. Baada ya kuwakamata tumechukua hatua kadhaa lakini baadhi yao wamelipa faini na wengine walikimbia kwa sababu walikuwa wanaendesha biashara hiyo kinyemela.
"Watu wanapaswa kutambua kuwa mashine hizi hazitakiwi kuendeshwa kwenye nyumba ya mtu, hazitakiwi kuendeshwa karibu na shule, hospitali, maeneo ya Usalama wa Taifa, maeneo yanayohusu watoto pamoja na sehemu ngumu kufikiwa na Jeshi la Polisi," alikumbusha masharti ya leseni za michezo hiyo.
Kiongozi huyo pia aliwataka wananchi kufuata sheria huku akionya wanaomiliki wa mashine wenye leseni kuendesha michezo hiyo pasi na kufuata sheria.
"Lakini pia nionye wale wate wanaoingiza mashine hizi kwa njia haramu nchini, sasa hivi tuko macho kila idara, tumejipanga kila kona kuhakikisha hilo halitokei. Nitoe onyo waache mara moja," alisisitiza.
Mkurugenzi Msaidizi wa Kiwanda cha Chilambo Generation Company limited, Benither Gidioni alisema shughuli yao kuu ni kuchakata taka hatarishi na kuzihifadhi ili zisilete madhara katika jamii.
"Sisi ni kampuni, tunajishughulisha na taka hatarishi, tunazivunjavunja, hasa za umeme na kuzihifadhi kama leo (juzi) unaona tumepokea mashine 300 toka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania. Kwa hiyo, tutazibomoa na baada ya hapo tutapeleka kwenye viwanda vya kuyeyusha taka
"Ombi langu watu wakiwa na taka, wasisite kuleta hapa, ni mahali sahihi kwa kuchakata taka hatarishi, tunahakikisha zinapotoka hapa haziwezi kuleta madhara. Kwa hiyo, taka za umeme na kemikali chafu hapa ndipo mahala pake kama walivyofanya GBT," alitamba.










