Kuwa na hali hiyo inayonyooshewa kidole, onyo limetolewa kwa wanafunzi wa shule za sekondari kujiepusha na unywaji pombe chini ya umri ili kulinda afya zao na kujihakikishia kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Kampeni hiyo muhimu iitwayo SMASHED iliyoanzishwa katika Shule ya Sekondari ya Msasani katika mapambano dhidi ya unywaji pombe chini ya umri, iko chini ya kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL).
Kampeni hiyo imezinduliwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Magori, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ambaye alisisitiza azma ya pamoja ya kulinda ustawi na mustakabali wa kizazi cha vijana wa kitanzania.
"Ni faraja kuona kampuni ya bia ikipigania dhidi ya unywaji pombe chini ya umri, SBL wanatoa mfano mzuri sana kwa jamii. Ninatumaini kwamba tunaweza kujifunza na kushirikiana nao ili kulinda vizazi vyetu vijavyo dhidi ya unywaji pombe chini ya umri," amesema.
Ameongeza kuwa programu hiyo inatumia tasnia ya uigizaji kuangazia suala linalojitokeza katika jamii la matumizi ya pombe chini ya umri na athari zake hasi kwa vijana walioko shuleni.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za kiafrika ambazo vijana wengi huanza matumizi ya pombe mapema katika umri mdogo.
"Utafiti uliofanywa mwaka 2019 katika mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro, ulibaini kuwa kiwango cha matumizi ya pombe miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari wenye umri wa miaka 15 na zaidi kilikuwa kati ya asilimia 12.9 kwa wasichana mkoani Mwanza hadi asilimia 63.9 kwa wavulana mkoani Kilimanjaro," amesema.
Amebainisha kuwa wakati kiwango cha matumizi ya pombe miongoni mwa wanafunzi wenye umri wa miaka 13 hadi 15, Mkoa wa Dar es Salaam kilikuwa asilimia asilimia 5.6.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo katika Shule ya Sekondari ya Msasani wilayani Moshi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi amesema, "SBL inafurahi kusaidia uanzishwaji programu ya SMASHED dhidi ya unywaji pombe chini ya umri kwani inaimarisha shughuli za kuhakikisha bidhaa zetu haziuuzwi au kutumiwa na watu walio chini ya umri wa miaka 18.
Amesema programu hiyo inahusisha utoaji mafunzo muhimu kuhusu athari hasi za kunywa pombe chini ya umri kwa vijana na jamii kwa ujumla.
"Programu hii inachanganya matumizi ya maonesho ya maigizo na ushiriki wa wanafunzi katika mazingira ya kujifunza yanayowapa motisha ili kuwajengea uwezo.
"Pia kuwajengea ujuzi na ujasiri wa kufanya uamuzi wenye dhamira nzuri na kuendelea kuwa na mitazamo chanya ya kujali na kutunza afya zao," amesema.
Anyalebechi amesema SBL iliandaa programu hiyo miaka miwili iliyopita ikitoa elimu kwa wanafunzi walio chini ya umri katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga ambapo kampuni hiyo iliwafikia zaidi ya wanafunzi 20,000 katika mikoa hiyo.









