Wanafunzi wanaolawitiana na kubakana shuleni waongezeka

11Mar 2024
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Wanafunzi wanaolawitiana na kubakana shuleni waongezeka

​​​​​​​JESHI la Polisi mkoani Morogoro limesema kuna ongezeko la vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyohusisha wanafunzi wenye umri chini ya miaka 18 wanaotendana ukatili huo wanapokuwa shuleni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alibainisha hayo mjini hapa alipochangia mada kuhusu vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyoongezeka mkoani humu wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Morogoro (RCC).

Alisema matukio ya vitendo vya ubakaji na ulawiti yanaongezeka kwa kasi mkoani Morogoro, waathirika wakubwa wakiwa ni watoto wakiwamo wanafunzi wenye umri wa kuitwa watoto

“Cha kusikitisha ni kuwa vitendo hivyo vingi watuhumiwa ni watoto chini ya umri wa miaka 18 kwa maana wenyewe kwa wenyewe wanafanyiana vitendo vya kulawitiana na kubakana,” alisema.

Kamanda Mkama ambaye hakuweka wazi takwimu za ongezeko la vitendo hivyo, alisema matuko hayo mengi yanafanywa kwenye maeneo ya shule na yanafanywa na wanafunzi wenyewe kwa wenyewe.

“Katika uchunguzi wetu tumebaini hawa wanafunzi wanalawitiana zaidi ya mtoto mmoja au mtoto mmoja analawiti zaidi ya mtoto mmoja,” alisema.

Kamanda Mkama alisema matukio hayo yamekuwa yanaongezeka siku hadi siku, hasa kipindi ambacho shule ndiyo kwanza zinakuwa zimefunguliwa; akiitaja miezi ya Januari, Februari na Machi kuwa kipindi hatari zaidi.

Alisema matukio hayo yanaongezeka nyakati hizo, yakiripotiwa kwao na waratibu elimu kata na madawati ya jinsia na watoto ya polisi.

Alisema athari za matukio hayo zinakuja kufahamika zaidi kuanzia miezi Januari hadi Machi, baadhi ya watoto wakibainika kuwa na ujauzito wanapopimwa afya zao.

Kamanda huyo alisema kuwa katika kipindi cha Novemba na Desemba, matukio hayo yanakuwa machache kutokana na wanafunzi kuwa likizo, wanakuwa chini ya uangalizi wa wazazi wao.

Kutatua tatizo hilo, Kamanda Mkama alisema Jeshi la Polisi linashirikiana na wadau wengine kutoa elimu shuleni kupitia dawati la jinsia.

“Sababu kubwa ya matukio haya ni mila na desturi zinazokiuka maadili mazuri kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Shule zinapofungwa kunakuwa na vigodoro (ngoma za asili) vingi,” alilalama.

Kamanda Mkama alisema wazazi kutokutoa ushirikiano kwa kwenda kutoa ushahidi mahakamani huku wakimalizana kifamilia na wahalifu ni sababu nyinyine ya kushamiri vitendo hivyo, hata kukwamisha jitihada za kumaliza matukio hayo.

Alisema polisi imeshapendekeza kuwa tukio ubakaji na ulawiti linapotokea, mara moja aliyefanyiwa kitendo hicho atoe shahidi mahakamani badala ya kusubiri muda mrefu kwa vile muda wa kusubiria unatoa mwanya kwa pande mbili hizo kumalizana.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema amekuwa akipatiwa taarifa na Kamanda wa Polisi Mkoa kila siku kuhusu vitendo vya ubakaji wanawake na watoto pamoja na ulawiti. Vimeshamiri mkoani mwake.

Malima alisema kutokana na kuwapo mfululizo wa matukio ya ubakaji wanawake, watoto na ulawiti, mkoa umejipanga kudhibiti matukio hayo na kuyakomesha.

Mkuu wa Mkoa alipandekeza kuitishwa kikao maalum na kumwalika Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima na timu yake kushiriki na kujadiliana kuwa na mkakati wa pamoja wa kudhibiti ukatili huo shuleni kwa kuangalia upungufu wa kisheria na kuwa na mpango endelevu wa utoaji elimu kwa jamii.

Januari 2020, Nipashe ilichapisha ripoti maalum kuhusu madhila ya watoto kulawitiana shuleni wilayani Mkuranga, mkoani Pwani. Ilithibitishwa na mamlaka za serikali kwamba vitendo hivyo haviko wilayani Mkuranga au Mkoa wa Pwani pekee, bali pia mikoani mingine nchini, vitendo hivyo vikitajwa kushamiri zaidi mikoa ya Tanga na Dar es Salaam.

Vilevile, Januari mwaka, gazeti hili pia liliripoti kuhusu wanafunzi kufundishwa kulawitiana wakiwa shuleni katika baadhi ya shule binfasi mkoani Kilimanjaro huku baadhi ya walimu mkoani humo wakinaswa na serikali wakipatiwa mafunzo ya vitendo vya ‘kisheni’.