Akiwa na angalizo mahususi kwa watendaji wenzake wa mahakama, Jaji Mkuu Juma ameanika vitendo vya unyanyapaa kwa kundi hilo, akiwataka majaji na mahakimu wanawake kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kwa kuwa wao ndiyo kundi linaloathiriwa zaidi na unyanyapaa huo.
Amesema kufanya mazoezi na kupuuza mashambulizi dhidi yao kwenye mitandao ya kijamii kunaepusha msongo wa mawazo unaowakuta wanapofanya uamuzi kwenye kesi mbalimbali.
Akizungumza katika kongamano la kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake jijini Dar es Salaam, Prof. Juma ametoa mfano wa yaliyomkuta kwa watu aliowakuta mahali kumkimbia, lakini hakuchukulia maanani na kutoathirika kisaikolojia.
“Hivyo, majaji na mahakimu wanapaswa kuzingatia hilo (kutotilia maanani unyanyapaa) na kufanya mazoezi mara kwa mara,” amesema.
Akirejelea utafiti uliofanyika Marekani kuhusu msongo wa mawazo na ustahimilivu kwa majaji wa Marekani, Prof. Juma amewataka watendaji wenzake wa mahakama kupambana na kikwazo hicho ili kufanya kazi zao vizuri.
Katika kongamano hilo ambalo pamoja na mambo mengine lilikuwa linaangazia tafakuri ya msongo wa mawazo kwa majaji na mahakimu wanawake, Jaji Mkuu amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti huo wa Marekani, vipo visababishi 37 vya msongo wa mawazo kwa majaji na mahakimu, vikijumuisha mashambulizi katika mitandao ya kijamii.
“Kuna jaji mmoja mwanamke, siku moja nilimwuliza ‘huwa ninaona unashambuliwa sana kwenye mitandao ya kijamii, unajisikiaje?’ Nilitaka kujua anahimili namna gani kwa sababu wakati mwingine wewe unafanya kazi yako kwa kufuata haki, lakini yaliyoandikwa katika mitandao ya kijamii yanakukatisha tamaa.
“Sisi wengine tuliishazoea usipoandikwa wiki nzima kusemwa vibaya, huwa hatujisikii vizuri kwa sababu nimeshazoea ubishi na kushambuliwa, wakati mwingine nilitaka kutayarisha mito ya kulalia iliyoandikwa Ibrahim Hamis Juma ili wale wanaonishambulia wawe wakilala usiku, wanataja Ibrahim Hamis Juma. Ni njia moja ya mbinu za kupambana na msongo wa mawazo,” amesema.
Jaji Mkuu ametaja visababishi vingine ni matokeo ya uamuzi unaotolewa katika kesi mahakamani, akifafanua kuwa katika kesi wakati mwingine mwenendo wa ushahidi unaotolewa hauridhishi, lakini hakimu hulazimika kutoa hukumu kutokana na ushahidi ulioletwa, jambo ambalo hupelekea msongo wa mawazo.
Pia amesema wapo watu wanaofungua kesi mahakamani wakiwa ni ndugu wa familia moja, lakini hutaka jaji au hakimu kukaa upande mmoja na asipofanya hivyo humtaka jaji au hakimu huyo kujitoa katika kesi, jambo ambalo mara nyingi humwathiri kisaikolojia baada ya kuona kuwa wanaoleta kesi wanamtaka kupindisha sheria na kusimama na kundi mojawapo.
“Sababu nyingine iliyotajwa inasababisha msongo wa mawazo kwa majaji ni aina ya migogoro wanayoletewa. Unaweza kukuta wadaawa ni wa familia moja, wanapambana na migogoro yao ya nyumbani, wanaileta mahakamani na wanataka wewe jaji uegemee upande mmoja au mwingine na ukijaribu kuwa katikati unazua uadui.
“Wakati mwingine unaambiwa ‘Mheshimiwa Jaji jitoe!’ Unapojitoa wakati wewe unajua unataka haki na upo sahihi, hili vilevile husababisha msongo wa mawazo na wengine hubeba huo msongo na kwenda nao nyumbani,” amefafanua Prof. Juma.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji wa Mahakama ya Rufani, Barke Sehel amesema kuna ongezeko kubwa la majaji, mahakimu na watendaji wengine wa mahakama wanawake tangu mwaka 1970 ambapo Jaji mstaafu Eusebia Munuo kwa mara ya kwanza aliingia katika mfumo wa mahakama nchini akiwa ni mwanamke pekee.
Amebainisha kuwa kwa sasa katika Mahakama ya Rufani kuna majaji wanawake 13 kati ya 35 waliopo huku katika Mahakama Kuu kuna majaji wanawake 38 kati ya 105 waliopo.
“Jaji Eusebia Munuo ndiyo mwanamke wa kwanza kabisa kuingia katika mahakama zetu, aliteuliwa kuwa hakimu mkazi wa kwanza mwanamke mwaka 1970 na wakati ule hapakuwa na mwanamke yeyote aliyekuwa na nafasi katika mahakama zaidi yake, yeye peke yake nchi nzima.
“Pia alikuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya juu kabisa katika mahakama zetu mwaka 2002 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
“Mwaka ule alipoteuliwa kulikuwa na jumla ya majaji tisa wa Mahakama ya Rufani, ndiye alikuwa mwanamke peke yake na pia ndiye mwanzilishi wa TAWJA, alipata shida kukianzisha kwa sababu Chama cha Majaji Wanawake Duniani kilitaka pawapo angalau majaji 10, hawakufikisha idadi, ikabidi waombe wachanganye na mahakimu ndipo wakakubaliwa,” amesema.










