Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Naibu waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, amesema kuwa idadi ya walioripotiwa kupata madhara kwa kula kiumbe hicho imeongezeka na kufikia watu 160.
Amesema waliofariki ni watoto chini ya umri wa miaka 10 na bado watu 18 kati ya 160 waliopata madhara wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Abdallah Mzee, kisiwani Pemba.
Amesema tukuo hilo limetokea Machi 6, mwaka huu katika Kijiji cha Kisiwa Panza, Kusini Pemba.
Hafidh alisema Wizara ya Afya imepiga marufuku ulaji wa nyama wa kiumbe huyo wa baharini ambaye huwa na sumu kali kutokana na vyakula wanavyokula wakiwa baharini.
"Wizara ya afya inawapa pole wale wote waliokula nyama hiyo na wale waliofariki. Niwaombe wananchi kuachana kabisa na ulaji wa kasa," amesema.
Amesema kuna aina saba ya kasa na kati ya hizo aina nne huwa ni hatari na wana madhara, hafai kuliwa lakini ni vigumu kumgundua kasa mwenye sumu kati ya aina hizo saba.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Faridi Mzee Mpatani, amesema kasa ana sumu inayotokana na aina ya majani na matumbawe yaliyopo baharini.
Amesema katika uchunguzi wamegundua kuwa sumu hiyo husababisha madhara katika mfumo wa ufahamu wa binadamu na husababishwa na mimea na vimelea vya baharini ambavyo hutumiwa na kasa kama chakula chao.
Amesema madhara ya sumu hiyo humsababishia binadamu kukosa nguvu, kupata ganzi, kutapika na kuharisha na kufariki dunia na kwamba watoto chini ya miaka 15 huwaathiri zaidi.
Amesema kuna baadhi ya viumbe baharini wanaweza kula mimea yenye sumu hiyo na wasilete madhara kwa binadamu.
Naibu Mkurugenzi kinga na elimu ya afya wa Wizara ya Afya, Fatma Mohamed Kabole, amesema wagonjwa hao pamoja na waliofariki ni kutoka katika familia tofauti.
Amesema baada ya kupata taarifa hiyo walifuatilia na kufika katika familia hizo na kugundua baadhi ya wagonjwa wamefichwa majumbani.
"Yawezekana idadi ya walioathirika wakaongezeka kwa sababu wananchi wanaficha taarifa ya waliokula nyama hiyo," amesema.
Hata hivyo, amesema Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuacha kula viumbe vya baharini vyenye madhara ikiwamo kasa na bunju kwa sababu hakuna tiba ya kudhibiti sumu ya viumbe hao.
Imedaiwa kuwa baadhi ya watu wanaokula nyama hiyo wanaamini inaongeza nguvu za kiume.









