Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Singida, Phaustine Ngunge, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 26 mwaka huu katika Kijiji cha Mitundu wilayani Manyoni mkoani hapa.
Alisema wahamiaji hao haramu ambao jumla walikuwa tisa walikuwa wakisafirishwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser ambalo namba za usajili hazijajulikana, akibainisha majeruhi walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa matibabu.
Ngunge alisema wahamiaji wanne ambao hawakujeruhiwa katika ajali hiyo, walikimbia na kwenda kusikojulikana lakini baada ya siku moja walijisalimisha katika Kituo cha Polisi Mitundu wilayani Manyoni.
Alisema waliofariki dunia katika ajali hiyo, miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida ambapo taratibu za mazishi zifanyika baada ya kupata kibali kutoka Ubalozi wa Ethiopia ama kuzikwa nchini au kusafirishwa.
Kuhusu majeruhi, alisema wametibiwa na kupona na kwamba hadi sasa wanashikiliwa na Jeshi la Uhamiaji ambapo kesho watuhumiwa saba wanatarajia kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuingia nchini bila kuwa na kibali.
Aliongeza kuwa dereva wa gari lililowasafirisha, ametoroka na hajulikani aliko na gari hilo lililotumika kuwasafirisha wahamiaji hao haramu linashikiliwa katika Kituo cha Polisi Mitundu.
Ofisa huyo wa Uhamiaji alisema katika mahojiano na wahamiaji hao, walisema wametumia miezi minane kutoka Ethiopia hadi kufika mkoani Singida.
Kufuatia tukio hilo, Ngunge alionya Watanzania wakiwamo askari kutojiingiza katika biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu kwa kuwa wakikamatwa, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
"Ninatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singida mnapomtilia shaka mtu ambaye siyo raia wa Tanzania, mtoe taarifa katika Jeshi la Uhamiaji na katika chombo chochote cha usalama," alisema.
Tukio hili limekuja siku chache baada ya askari mkoani Mbeya kukamatwa wakituhumiwa kusafirisha wahamiaji haramu.










