Mwinyi aanika mafanikio miaka miwili

06Nov 2022
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Mwinyi aanika mafanikio miaka miwili

​​​​​​​RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema licha ya changamoto ya  UVIKO-19 na vita vya Russia na Ukraine, ndani ya uongozi wake wa miaka miwili ukusanyaji wa mapato umeongezeka katika serikali yake.

​​​​​​​Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana Ikulu, Zanzibar wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka miwili ya uongozi wake tangu alipochaguliwa mwaka 2020.

Alisema ongezeko hilo la mapato linatokana na idadi kubwa ya watalii wanaofika Zanzibar. Alisema hali hiyo imeanza kurejea kama ilivyokuwa kabla ya janga la UVIKO-19.

Rais alisema anajivunia uchumi kuimarika licha ya janga la UVIKO-19 na vita vya Ukraine na Russia vinavyoikumba dunia na kusababisha uchumi kusimama na sasa kuna kila dalili hali ya uchumi kurejea katika hali yake ya nyuma na kuvuka malengo.

Alisema katika sekta ya utalii wageni wameongezeka na kwa mara ya kwanza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume umekuwa namba moja kwa kuingiza watalii wengi na kuakisi mapato yanayopatikana kutokana na uingiaji wa wageni.

“Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wakati naingia madarakani walikuwa wanategemea mishahara kutoka serikali na serikali ikitoa Sh. milioni 400 kila mwezi kwa ajili ya kulipa mishahara. Nafurahi  kusema katika kipindi cha miezi mitatu, robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, mwaka huu, wamevunja rekodi ya mapato kwa kuingiza Sh. bilioni 6.7,” alisema.

Dk. Mwinyi alisema kuna kila sababu ya kujivunia mipango ya kukusanya mapato vizuri ili kuleta maendeleo. Alisema ukusanyaji wa fedha ni mzuri katika serikali yake na imetokana na hatua zilizowekwa ikiwemo mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, ndani ya miaka miwili ya uongozi wake, pia amefanikiwa kutekeleza maridhiano ya kisiasa ambayo yamefungua milango ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi katika sekta mbalimbali.

Alisema maridhiano hayo yanatokana na hali ya amani na usalama lakini pia ushirikiano kati ya viongozi wakiwamo wanasiasa na wananchi.

Mafanikio mengine, alisema ni kuongezeka kwa uwekezaji na miradi iliyosajiliwa ndani ya miaka miwili ni 181 yenye thamani ya dola bilioni tatu.

Miradi hiyo itazalisha ajira 11,289 na kituo cha uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imeimarisha huduma zao na cheti cha uwekezaji sasa kinatolewa ndani ya muda wa maa 24 endapo mwekezaji atatimiza masharti yanayotakiwa.

Alisema hatua hiyo itaendeleza kukuza uchumi wa nchi kwa sababu uchumi unategemea fedha za wawekezaji kutoka nje.

Kuhusu miradi ya maendeleo alisema hospitali za wilaya 10 zinaendelea kujengwa, ujenzi wa shule za gorofa, miradi ya maji na barabara ambapo ikikamilika huduma zitakuwa bora.

Alisema serikali yake imesimamia suala la utawala bora ikiwemo kutoa hadharani ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na hatua kuchukuliwa kwa wale wote waliotajwa katika ripoti hiyo kuhusika na ubadhilifu wa umma.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyobaki miradi mikubwa inatarajiwa kutekelezwa ili kubadilisha uchumi wa Zanzibar ikiwemo ujenzi wa bandari ya Mangapwani, ujenzi wa barabara kuu ikiwemo ya Kisauni-Fumba, ujenzi wa barabara za ndani zenye kilomita 200 na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.