Hali hiyo inatokana na kasi ya kukua kwa Teknolojia na kuongezeka kwa utandawazi ambao umechochea kasi ya mabadiliko ya soko la ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako wakati akifunga mafunzo kwa Wadadisi na Wasimizi wa Utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2024 yaliyofanyika mjini Morogoro.
Utafiti huo utahusisha Wadadisi 139,wasimamizi 26 ambao ni Mameneja wa takwimu wa mikoa utafanyika kwa muda wa miezi 12 ili kuwezesha kupima kikamilifu menendo ya ajira na ukosefu wa ajira kwa vipindi au misimu yote ya mwaka .
Profesa Ndalichako amesema Serikali nia ya kufanya utafiti huo ni kutokana na Serikali inahitaji kupata takwimu za kina za soko la ajira zitakazoakisi hali halisi kwaajili ya kufanya maamuzi yenye tija zaidi.
ProfesaNdalichako amesema lengo kuu la utafiti ni kupata viashiria vya soko la ajira nchini,kiwango cha ukosefu cha ajira , kiwango cha ajira isiyotimilifu,kiwango cha nguvu kazi ,kiwango cha jjira mbayá kwa watoto na kiwango cha ajira kwa aina ya kazi .
Amesema mpango umelenga kuisadia Serikali kuweka mikakati ya kufikia malengo iliyojiwekea ifikapo Mwaka 2025 kuzalisha ajira milioni nane ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya 2020-2025.
Waziri Profesa Ndalichako amesema mpango pia inadhihirisha dhamira ya Serikali inahakikisha inapanga mipango ya maendeleo kwa kuzingatia takwimu sahihi ili kukuza uchumi pamoja na soko la ajira.
Amesema kutokana na umuhimu huo Serikali inahitaji kupata takwimu za kina za soko la ajira zitakazoakisi hali halisi kwa ajili ya kufanya maamuzi yenye tija zaidi.
Profesa Ndalichako amesema matokeo ya Utafiti huo yatatumika kupima na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Pia amesema matokeo ya utafiti huo yatasaidia kupima utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na pia yatatumika kupima utekelezaji wa programu mbalimbali za kupima ukuzaji ,ujuzi na uzalishaji wa fursa za ajira.
Nae Mtakwimu Mkuu wa Serikali,Dk Albina Chuwa,amesema utafiti huo utafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ,ambapo kwa mikoa ya bara itafanyika kwenye maeneo ya kuhesabia 441 ambayo yamechaguliwa kitalaamu kuwakilisha maeneo mengine yote nchini.
Ameshukuru wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwaajili ya kufanikisha utafiti huo.
Nae Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara,Spika Mstaafu ,Anne Makinda,amesema takwimu zinaonyesha asilimia 55.4 ni nguvu kazi za Taifa lakini hakuna uhalisia hivyo kupitia utafiti huo utasaidia kuleta uhalisia ili kuisaidia serikali kufanya maamuzi.










