TECEC lawanoa wazazi ulinzi,malezi kwa watoto

04Mar 2024
Vitus Audax
Mwanza
Nipashe
TECEC lawanoa wazazi ulinzi,malezi kwa watoto

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Tanzania Early Childhood Education (TECEC) limeendesha semina kwa wazazi kutoka kata ya Luchelele, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza...

...ikililenga kutoa elimu kuhusu ulinzi, malezi na makuzi bora kwa watoto wenye umri kuanzia miaka Sifuri hadi Minane (0-8), hususani katika nyanja ya utambuzi, uelewa kielimu, na afya.

Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa TECEC Joel Elphas amesisitiza umuhimu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao kwa kuwe mkazo zaidi kuanzia mama akiwa Mjamzito mpaka mtoto anapofikisha umri wa miaka minane ili ubongo na Afya ya mtoto viwe imara.

"Wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanapata malezi bora na wanapewa elimu sahihi. Malezi yanayoanzia utotoni yanaweza kuwa na athari kubwa katika maisha ya mtoto hata baadaye." amesema Elphas

Amesema TECEC kupitia Mradi wa Tuwaandae Pamoja inaendelea na juhudi zake za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa malezi bora ya watoto na inawahimiza wazazi kuzingatia mahitaji ya watoto katika kila hatua ya ukuaji wao ikiwa ni pamoja na kuzingatia lishe. 

Mtaalamu wa Utengenezaji wa zana za kujifunzia kwa watoto na Mratibu wa Mradi wa Tuwaandae Pamoja Ester Macha ameshauri kuhusu namna ya kuandaa mazingira bora ya kujifunzia nyumbani. Amesema, "Ni muhimu kuwa na zana za kujifunzia ambazo zinachochea ubunifu na ujifunzaji wa watoto. Wazazi wanaweza kutumia vifaa vya kawaida nyumbani kama magazeti, karatasi, na rangi kuwasaidia watoto kujifunza kwa njia ya kucheza."

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Luchelele Marietta Mauta amesema upo umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na serikali katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora ili kuwa na Taifa lenye vijana wenye fikra chanya kwaajili ya maendeleo kwa ujumla.

Amesema, "Ni lazima jamii ijumuike katika suala la malezi ya watoto na kushirikiana na serikali kuboresha mazingira ya malezi. Watoto wanahitaji upendo, usalama na msaada wa kielimu ili waweze kukua na kufikia malengo yao."

Semina hii ilitoa fursa kwa wazazi kujifunza mbinu za malezi bora na kuuliza maswali kuhusu malezi ya watoto wao. Wazazi walionyesha shauku kubwa na ahadi ya kutekeleza mafunzo waliyopata katika malezi yao ya kila siku.