Mdoe: Wazazi msifiche watoto wenye ulemavu ndani

04Mar 2024
Maulid Mmbaga
Nipashe
Mdoe: Wazazi msifiche watoto wenye ulemavu ndani

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani akieleza kuwa kwa kufanya hivyo wanajiongezea mzigo na kuwafanya watoto wazidi kuwa tegemezi.

Ametoa wito huo leo mkoani Dar es Salaam katika hafla ya ugawaji wa vifaa saidizi kwaajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Sekondari Pungu, vikiwamo viti mwendo 160, kompyuta mpakato 20, tableti nane, projekta mbili, magodoro 26 na mashine ya kufulia,

 

Amesema tatizo la kuficha watoto ndani kwa baadhi ya wazazi bado lipo nchini, na kwamba endapo wataachana na tabia hiyo na kuwapeleka watoto hao shule ili wapate usaidizi itawasaidia kufikia malengo yao ya kielimu, akijitolea mfano yeye ambaye wazazi wake wanamtegemea kwa sasa licha ya ulemavu aliokuwa nao, ikiwa ni moja ya manufaa ya kupelekwa shule.

 

“Mimi nawasisitiza wasifiche watoto nyumbani kwani ndio watakuwa mzigo kwao, lakini wakiwatoa na wakaenda shuleni wataweza kufundishwa, kuweza kujitegemea na hata kufanya shughuli za kujiingizia kipato.

 

“Atakapofika shule atafanyiwa tathimini kama anaweza kusoma na wenzake na kama uhitaji wake ni mkubwa anatakiwa kupelekwa kwenye shule maalumu zaidi tunazo hizo pia na serikali inapeleka vifaa, walimu na mahitaji mengine maalumu kuwawezesha wanafunzi hao kusoma,” amesema Mdoe.