Meneja wa TANROADS mkoani humo, Motta Kyando, amesema fedha hizo zimetumika kurejesha mawasiliano ya barabara kwa kujenga upya madaraja mbalimbali, likiwamo la Daraja la Biriri lililoko eneo la kwa Wasomali Wilaya ya Siha.
Amesema daraja hilo limekuwa na desturi ya kufurika maji wakati wa msimu mvua na kisha kukata mawasiliano katika Barabara Kuu ya Moshi/Arusha. Daraja hilo limejengwa kwa Sh.milioni 990.
Amesema daraja lingine lililojengwa ni la Hingiriri lililopo Barabara ya Mwembe/Myamba/Ndungu, ambalo limeigharimu TANROADS Sh. milioni 246.
Kadhalika ametaja Daraja lingine ni la Kikelelwa lililopo Barabara ya Bomang’ombe/Sanya Juu/Kamwanga/Tarakea Polisi katika Wilaya ya Rombo, ambalo limetumia Sh. milioni 436.
Aidha, Kyando, amesema kuwa mvua hizo ziliifanya TANROADS kurejesha huduma ya mawasiliano ya barabara kwa kulijenga upya Daraja la Marangu Mtoni, lililopo Barabara ya Marangu Mtoni/KINAPA, kwa gharama ya Sh. milioni 549.
Daraja hilo liliathiriwa na mvua hizo na kuharibika, licha ya ukweli kwamba lilikuwa finyu na halikuwa na uwezo wa kuruhusu magari mawili kupishana.
Amesema mbali na madaraja hayo pia serikali ilitoa Sh. bilioni 1.722 kwa ajili ya kurejesha mawasiliano na kufanya matengenezo ya miundombonu katika maeneo yaliyoathiriwa na maparomoko ya miamba kwenye Barabara ya Mwembe/ Myamba/ Ndungu, Wilaya ya Same.
“Mvua za El-nino, zilisababisha kukatika kwa mawasiliano katika barabara kuu eneo la Hedaru (Same), ambayo ilisomba magogo, mchanga na uchafu sehemu za milimani na kuziba Daraja la Hedaru na kusababisha maji kufurika barabarani.
Vilevile, serikali ilitoa Sh. milioni 160 za kurejesha mawasiliano katika eneo hilo la Hedaru lakini pia ilitoa Sh. bilioni 1.6 kurejesha mawasiliano na kufanya matengenezo maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko katika Barabara ya Lembeni/ Kilomeni/ Lomwe.” amesema Motta.
TANROADS inahudumia barabara zenye urefu wa kilometa 1,098.83 mkoani Kilimanjaro zikijumuisha kilomita 292.74 za barabara kuu, huku kilomita 806.09 zikiwa ni barabara za mkoa.
Barabara za lami zinazomilikiwa na wakala huyo ni kilomita 518.27 na za changarawe kilomita 580.56.









