Mkemia Mkuu atoa ripoti tope la mgodi lililovamia wananchi

13Nov 2022
Marco Maduhu
Kishapu
Nipashe Jumapili
Mkemia Mkuu atoa ripoti tope la mgodi lililovamia wananchi

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC) limesema maji na tope yaliyotokana na kubomoka kwa kingo za bwawa la Mgodi wa Williamson Diamonds hayajaleta athari kwa mazingira na viumbe hai baada ya kupokea uchunguzi wa awali kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samwel Gwamaka.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samwel Gwamaka alibainisha hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ambayo yameathiriwa na maji na tope la bwawa hilo.

Alisema uchunguzi wa awali kutoka kwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali haujaonyesha athari zozote kwa mazingira na viumbe hai na kuwataka wananchi waliokumbwa na tukio hilo kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea na uchunguzi zaidi.

"Sampuli zilizopelekwa kwa Mkemia Mkuu zimeonyesha maji na tope hili halijaleta athari kwa mazingira na viumbe hai. Tunasubiria ripoti ya Tume ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ili tuweze kuchukua hatua zingine za kisheria," alisema Dk. Gwamaka.

Mkurugenzi huyo alisema mgodi huo utawajibika kulipa fidia kwa wananchi waliopatwa na janga hilo pamoja na kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa ikiwamo mashamba ya wanachi na nyumba ambazo zimepatwa na kadhia hiyo.

"Uharibifu wa mazingira uliosababishwa na tukio hili ni mkubwa, ni lazima wawajibike kuhakikisha mazingira yanatunzwa, hatua walizochokua za kusimamisha shughuli za uzalishaji na matumizi ya bwawa zinapaswa kuzingatiwa ili lisije kuleta madhara zaidi kwa wananchi," alisema.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Williamson Diamods, Ayoub Mwenda alisema kuwa kwa sasa wanaendelea kujenga uzio ili kuyadhibiti maji hayo yasisambae kwenye makazi ya watu hususani wakati huu ambao mvua imeanza kunyesha kwa wingi mkoani Shinyanga.

"Tunajenga matuta ili kuyadhibiti maji haya yasiendelee kusambaa, wataalamu wetu wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha maji hayo yanadhibitiwa," alisema Mwenda.

Aliongeza: "Mpaka sasa mgodi unaendelea kuwahudumia waathirika wa tukio hili wapatao 115 wakati tunasubiria majibu ya tume na tutahakikisha wanapata stahiki zao zote ikiwamo chakula na malazi huku watoto wao nao wakipelekwa shuleni kama kawaida."

Baadhi ya wakazi ambao wameathirika na tukio hilo, akiwamo Juma Masele, waliishukuru serikali kwa kuchukua hatua  dhidi ya tatizo hilo na kuiomba kuwasaidia eneo lingine ili waendelee na kilimo wakati huu ambao mvua imeanza kunyesha.

"Baadhi yetu ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini, tunaomba tupatiwe eneo lingine ili tuweze kuendelea na kilimo kwani kuendelea kukaa kwenye kambi hii wakati mvua inanyesha itakuwa tunapoteza muda," alisema Masele.

USULI NA HISTORIA

Inaporejewa historia ya uchimbaji madini Tanzania, kuwapo almasi kwenye eneo la Mwadui kuligunduliwa mwaka 1940 na raia wa Canada, Dk. John Williamson, mtaalamu wa jiolojia aliyekuwa amebobea katika masuala ya madini.