Hatua hiyo imekuja kutokana na Mbunge huyo kushindwa kuthibitisha tuhuma za ufisadi wa sh. bilioni 238 alizotoa dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria.
Kabla ya kumakiza kwa kikao cha asubuhi jana, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema Kanuni ya 63 (6), inamtaka mbunge kusema ukweli juu ya jambo lolote kwa kutoa uthibitisho kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge.
Alinukuu pia Kanuni ya 63 (8) inayosema: “Endapo hadi kufika mwisho wa muda ambao mbunge amepewa kuthibitisha jambo au kanuni au maenelezo yake, atakataa, au atashindwa kuthitisha na kuliabisha Bunge na kama atakataa kufuta kauli, usemi au maelezo yake, basi Spika atamwadhibu Mbunge huyo asihudhurie vikao vya bunge visivyozidi vitano”.
Baada ya maelezo hayo, Chenge alimtaka Kishoa kufuta kauli yake aliyoitoa Jumatatu wiki hii.
Baada ya kupewa nafasi hiyo, Kishoa alisema: “Ahsante Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba, sitafuta kauli yangu kwa sababu Mwakyembe hajathibitisha.”
Baada ya kukataa kufuta kauli hiyo, Chenge alisema “Kwa kuwa kanuni hii inanitaka kumsimamisha Mbunge kwa siku zisizozidi tano na kwa kuwa tumebakiwa na siku mbili tu kabla ya kumaliza mkutato wa Bunge, basi namsimamisha Jessica Kishoa kukuhudhuria vikao viwili vya Bunge kuanzia sasa hivi. Naomba utoke nje. Nakutaka utoke nje....” alisema Chenge.
Wakati Kishoa anatoka nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wa upinzani walimshangilia huku wa CCM wakimzomea: “mwongo, mwongo…”
NJE YA BUNGE
Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, mbunge huyo alisema atabaki na msimamo wake na kuwa ataendeleza mapambano dhidi ya suala hilo kwa sababu anahudumia wananchi.
Alisema aliomba kupewa taarifa hizo na kamati ya bunge inayosimamia reli lakini akaambiwa kuwa ripoti iliyokuwa imewasilishwa kwenye kamati hiyo, imerudishwa serikalini.
“Niliandika barua kwenda PPRA kupitia ofisi ya spika lakini sijapata majibu,” alisema.
Alisema ana uhakika kuwa kwenye suala hilo kuna tatizo kwa sababu malipo yalilipwa kwa asilimia 100 kabla hata mabehewa hayajafika nchini.
BARUA KWENDA PPRA
Gazeti hili lilifanikiwa kuiona Barua ambayo Mbunge huyo aliiandikia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Februari 2, akiomba kupatiwa ripoti ya mwisho ya uchunguzi kuhusu uagizaji mabehewa.
Katika sehemu ya barua hiyo anasema: “Machi 2015, Mamlaka yako iliwasilisha ripoti ya awali kuhusu uchunguzi katika sakata la uagizaji mabehewa ambapo pamoja na mambo mengine ilionyesha mabehewa yaliyoagizwa yalikuwa chini ya kiwango.
Sheria ya Manunuzi ilikiukwa, uchunguzi wa kina kuhusu kampuni ya Hindustan Engineering Ltd iliyopewa zabuni hiyo haikufanyiwa uchunguzi kuhusu uwezo na rekodi yake kabla ya kupewa kazi hiyo (due deligency),” inasema barua hiyo.
Katika barua yake hiyo, alinukuu Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema kazi ya Bunge ni kusimamia na kushauri serikali.
“Na kwa kuzingatia Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge (CAP296), R. E 2002. SEC10, Imenipa haki Mbunge kupatiwa taarifa na mamlaka za serikali kwaajili ya ufanisi wa utendeji wangu.
Na kwa kuwa, jana (Februari Mosi) nikichangia bungeni niligusia sakata la ufisadi katika uagizaji mabehewa feki. Kwa barua hii, naomba kupatiwa ripoti ya mwisho (final report) kuhusu uagizaji wa mabehewa kwa Kadiri ya uchunguzi wa mamlaka yako.
Nipatiwe kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa pili unaohitimishwa Februari 5, 2016,” inasema barua hiyo.
TAARIFA YA PPRA
Nipashe ilifanikiwa kuona sehemu ya taarifa ya Shirika la Reli (TRL), katika utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN), ambayo inasema ilinunua mabehewa 25 ya kubebea kokoto na yaligharimu Sh blioni 4.316 na kwamba yaliwasili nchini Julai, 2014.
Taarifa hiyo inaonyesha pia kuwa Sh. bilioni 284.952, kiasi kinacholingana na kile ambacho Kishoa alikitaja ni bajeti ya maendeleo ambayo TRL imezipata kati ya mwaka 2011/12 mpaka 2015/16 kati ya Sh 487.964 zilizoidhinishwa na bunge.
SAKATA LILIVYOANZA
Akichangia mjadala huyo, Kishoa alisema taifa limeingia hasara la sh. bilioni 238 kwa kununua mabehewa mabovu na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi kipindi hicho (Dk Mwakyembe) yuko bungeni ameshindwa kuwasilisha ripoti ya sakata hilo.
“Kazi iliyopo ni kupanga mipango ambayo haitekelezeki mpaka leo tunahitaji ripoti ya mabehewa iko wapi. Haipatikani na Dk. Mwakyembe yupo hapa hili nalo ni jipu,” alisema
Kutokana na kauli hiyo, Dk. Mwakyembe aliomba ufafanuzi kuhusu utaratibu kwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Mary Mwanjelwa, ambapo alisema kwa kutumia kanuni ya 63 (3) mbunge huyo amesema uongo na serikali haijawahi kutumia zaidi ya bilioni 60 kununua mabehewa na kwamba mbunge huyo amelidanganya bunge na kumtaka atoe uthibitisho juu ya jambo hilo na akifanya hivyo atajiuzulu.
Dk. Mwakyembe alisema ni vyema watu wasigeuze bunge kuwa kijiwe cha kubishana na mambo yasiyo ya msingi.
Kabla Mwenyekiti wa bunge kutoa nafasi Kishoa kutoa uthibitisho, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alitumia kifungu cha 63 (4) akisema kwa mujibu wa kifungu hicho anayepaswa kutoa uthibitisho ni Dk. Mwakyembe ambaye anamtuhumu mbunge huyo.
Kauli hiyo ya Mdee ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, kusimama na kusema ushahidi au uthibisho ambao Mdee amemtaka Dk. Mwakyembe atoe ameshaueleza na kusema serikali haijawahi kununua mabehewa ya zaidi ya Sh. bilioni 60.
Alisema aliyedanganya bunge ndiye anayetakiwa kuwasilisha uthibitisho kwa kuwa waziri ameshatoa ufafanuzi. Hatua hiyo ilimfanya Mwanjelwa kumwagiza Kishoa kumpelekea uthibitisho ndani ya siku tatu kuhusiana na tuhuma hizo.
0000










