Kadhalika ameagiza kesi 26 za kukutwa na nyara za serikali yakiwamo meno na pembe za ndovu ambazo watuhumiwa wanadaiwa kukutwa na vilelezo moja kwa moja, Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuhakikisha wanashirikiana kumaliza kesi hizo.
Rais Dk. Mgaufuli alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na mwaka mpya wa mahakama.
“Mheshimiwa Jaji Mkuu, leo hii kuna kesi 42 zinazowakabili wakwepa kodi tangu mwaka 2010 lakini zikiamuliwa hizo serikali yetu inapata Sh. trilioni moja. Nawaahidi majaji na mahakimu mkizitolewa kesi hizo uamuzi, Sh. bilioni 250 nitazitoa mahakamani,” alisema Rais.
Kuhusu utendaji wa mhimili huo, alisema mahakama kwa ujumla wanafanya kazi ya Mungu na katika mazingira magumu kwa ajili ya Watanzania wote kutokana na mahakimu kukosa usafiri na wakati mwingine kulazimika kutumia usafiri wa pikipiki kwenda kutoa haki kwa wananchi.
Alisema ili mazingira ya utendaji kwa mahakimu yaboreshwe, watumishi wanaojiendeleza kwa fedha za mahakama kuanzia sasa watasoma kupitia bodi ya mikopo.
“Nileteeni orodha ya majina ya watumishi wanaotaka kujiendelea niwaunganishe kwenye bodi ya mikopo waweze kupata elimu wanayoitaka ili fedha zinazotumika kuwaendeleza watumishi kutoka mfuko wa mahakama ziende kununua magari na kuboresha mazingira ya kazi ya mahakimu wanaofanya kazi katika hali hatarishi” alisema.
MAHAKAMA YA MAFISADI
Kuhusu kuanzishwa kwa mahakama ya mafisdadi na wahujumu uchumi, Rais Dk. Magufuli alisema machakato huo ushughulikiwe haraka kwa kuwa ni muhimu sana katika kupambana na kutokomeza mafisadi.
Alisema mtu anapokamatwa na vielelezo hakuna sababu ya kuchelewesha kesi na DPP na polisi wakishirikiana nchi itakwenda mbele.
“Ndoto yangu ni kuundwa mahakama ya mafisadi. Harakisheni, wanaendelea kuichezea nchi hawa. Niliahidi kuwa nikipata urais lazima iundwe mahakama hiyo. Mimi ni mkweli naamini hata nikifa nitakuwa rais wa malaika,” alisema
Aidha aliiahidi mahakama kuipatia Sh. bilioni 12.7 kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo ndani ya maendeleo.
Naye Jaji Mkuu Mohhamed Chande alisema mahakama inaendelea na mchakato wa kuanzisha mahakama ya mafisadi na uhujumu uchumi na kwamba itakuwa na nguvu na yenye uwezo wa kurekebisha mafisadi wakubwa inayotarajia kuanza kazi mapema mwaka huu.
Alisema mahakama hiyo ambayo iko mbioni kuundawa itakuwa kitengo cha Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo itasikiliza kesi zilizokamilika upelelezi wake.
Akifafanua zaidi kuhusu mahakama hiyo alisema rufani za kesi hizo zitaendeshwa katika utaratibu maalumu ili haki iweze kupatikana kwa pande zote mbili.
Aidha, alisema katika uundwaji wa mahakama hiyo, Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na DPP waimarishwe ili kuboresha hatua hiyo muhimu na kwamba baadhi ya sheria ziboreshwe ili kesi hizo ziende kwa wakati.
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema vyombo vinavyohusika na upelelezi na uchunguzi vikiwamo polisi, Takukuru na tume ya kuzuia dawa za kulevya, vina nafasi muhimu katika kuhakikisha utoaji haki inawalenga wananchi.
Alisema wajibu wa vyombo hivyo ni kuhakikisha mhalifu aliyetenda kosa ndiye anayekamatwa na kuchunguzwa na kisha kufikishwa mbele ya mahakama ili kuepuka kubambikia watu kesi kwa makosa ambayo hawakutenda.
Mahakama ya mafisadi yaiva, yapewa angalizo
05Feb 2016
Hellen Mwango
Nipashe
Mahakama ya mafisadi yaiva, yapewa angalizo
RAIS Dk. John Magufuli ameagiza mahakama nchini kusikiliza na kuzitolea uamuzi kesi 42 zinazowahusu wakwepa kodi, ambazo zikimalizika serikali itapata Sh. trilioni moja.










