Mbowe ni mnufaika mkubwa wa maridhiano -Makonda

14Jan 2024
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mbowe ni mnufaika mkubwa wa maridhiano -Makonda

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amesema Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ni mnufaika mkubwa wa maridhiano ambayo yamemfanya akawa huru na kesi zake za kisiasa.

Paul Makonda.

"Kwa masikitiko makubwa jana tumepata nafasi ya kumsikia kaka yetu Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA akituhumu na kutoa kauli za kuzalilisha na kufedheesha na kutweza utu wa Kiongozi wetu bila kujali dhamira njema aliyoonyesha Mwenyekiti wetu wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa Umoja na Mshikamano katika Taifa letu" amesema Makonda

"Taifa hili kwa mara ya kwanza limeshuhudia haki ikisimamiwa kikamilifu ikiwa pamoja na jitihada binafsi za Mwenyekiti wetu wa CCM na Rais alizozifanya katika kuunda tume ya haki jinai kupitia mambo kadhaa wa kadhaa ili kuhakikisha Mtanzania anapata haki yake bila kujali rika, elimu kipato, kabila , dini na hata kule alipotokea"

Makonda amesema Mbowe ametamka maneno mazito upo wakati wameyatafakari nakuona kuna haja ya kumjibu kwani ameeleza umma mambo ya uongo licha ya kuwa mnufaika mkubwa wa maridhiano.

"Moja ya hoja kubwa aliyosimama nayo katika mchakato huu wa mswaada wa sheria tatu (Sheria ya vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi yenyewe) amediriki kueleza hadharani ya kwamba mapendekezo yaliyotolewa na kikosi kazi kilichoundwa na Rais kwa mapenzi mema , mapendekezo yaliyotolewa na CCT  na  yaliyotolewa na baadhi ya vyama vya siasa kwamba yote yamepuuzwa ...jambo hilo sio kweli hata kidogo," amesema Makonda

Makonda amesema Mbowe anafahamu katika mapendekezo 84 yaliyotolewa mapendekezo 63 yote yamechukuliwa na yapo kwenye msawaada ambao hatua za kisheria zinaendelea katika kuunda kwa sheria.

"Mbowe ni mnufaika mkubwa wa maridhiano ambayo yamemfanya akawa yupo huru na kesi zote za kisiasa kuachiwa huru bila masharti na yeye mwenyewe na chama chake na vingine kufanya mikutano ya hadhara bila kubugudhiwa tena kwa ulinzi mkali chini ya jeshi la polisi kuhakikisha dhamira ya Rais Samia inatimia si tu kwa vyama vya siasa bali kwa Watanzania wote"