Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo, amesema kuwa, katika mapambano hayo askari polisi walilazimika kutumia mabomu na risasi, baada ya wabeba mkaa kukaidi kujisalimisha na kuwashambulia askari na maofisa wa misitu kwa mapanga.
Amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana wakati askari polisi kwa kushirikiana na maofisa wa misitu wakiwa doria ya kuzuia uvunaji haramu wa mazao ya misitu.
Kamanda Lutumo amesema katika doria hiyo watuhumiwa saba walikamatwa na magunia 70 ya mkaa pamoja na pikipiki 26.
Amesema awali waliokuwa katika operesheni hiyo walikutana na kundi la watu wakiwa na pikipiki zilizobeba mkaa na walipotakiwa kujisalimisha walikaidi na kuanza kuwashambulia askari polisi na maofisa wa misitu kwa mapanga.
“Kutokana na hali hiyo polisi walijibu (mapigo) kwa kufyatua mabomu ya kishindo na risasi za moto hewani, lakini watu hao wakiendelea kukaidi na kuendelea kukabiliana na askari wakitumia mapanga na visu.
“Katika mapambano hayo askari namba G.7247 koplo Ramadhani (37) amejeruhiwa kwa kukatwa na panga mikononi na kichwani ambapo alikimbizwa Hospitali kwa matibabu.
Kamanda huyo amesema kutokana na tukio hilo, Frank Boniface (33), alikutwa amefariki dunia eneo la tukio na uchunguzi wa kifo hicho unaendelea.
Wakizungumzia tukio hilo, madereva wa bodaboda wamesema tukio hilo lilitokea majira ya saa sita usiku wakati wakiwa kwenye safari wakitokea msituni ndipo walipokutana na gari ambalo lilikuwa na askari wa misitu ambao walifyatua risasi.
Abison Songa, mmoja wa madereva pikipiki ambao waliamua kusitisha safari yao katika Kijiji cha Kwala baada ya tukio hilo, amesema wamekuwa wakikumbana na matukio hayo mara kwa mara na kudai kuwa, baadhi yao hupoteza maisha.
Songa ameiomba serikali kuridhia kuwapatia vibali vya kusafirisha mkaa kama vinavyotolewa kwenye magari na toyo ili kuepusha sintofahamu za mara kwa mara.
Sabas Enock, ameshauri suala hilo litafutiwe ufumbuzi kwa kuwa, limekuwa chanzo cha ongezeko la majeruhi madereva wa bodaboda na vifo.
Katibu wa umoja wa madereva bodaboda wabeba mkaa hao, Ramadhani Msemakweli, amesema tukio hilo ni la tano kutokea na sababu kubwa ni kutokana na kukosa vibali vya biashara hiyo.
Ramadhani amesema kwa sasa idadi yao inafikia 200 na hawana kazi ya kufanya zaidi ya biashara hiyo ya mkaa, huku wakala huo ukisisitiza kuachana na biashara hiyo badala yake watumie magari badala ya bodaboda.
“Sisi tuko tayari kulipa ushuru unaotakiwa wa halmashauri na serikali kuu na tuko tayari kupunguza ukubwa wa magunia kama itahitajika kufanya hivyo. Cha kushangaza ni kwamba, tatizo hili ni kwa Mkoa wa Pwani pekee, wakati ipo mikoa mingine ambayo kuna madereva wanaosafirisha mkaa kama sisi,” amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwala. Salumu Bai. amesema usiku wa kuamkia jana, alisikia milio ya risasi na asubuhi alipokwenda eneo la tukio alikuta mwili wa kijana mmoja wa bodaboda anayedaiwa kupoteza maisha kwa madai ya kupigwa risasi na askari wa misitu.
Januari, mwaka huu, mvutano baina ya askari sita wa TFS na vijana wanne wabeba mkaa ulioibuka eneo la Tegeta Machinjioni, Dar es Salaam, ulisababisha asiyehusika kujeruhiwa kwa risasi kwa madai ya askari hao kufyatua risasi na kumjeruhi muuza nyama.