Mbaroni tuhuma za kuvunja nyumba usiku na kupora

11Sep 2022
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mbaroni tuhuma za kuvunja nyumba usiku na kupora

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu 10 wanaotuhumiwa kuvunja nyumba za wananchi wa Kinyerezi Kibaga jijini Dar es Salaam na kupora mali mbalimbali.

Wiliam Mkonda.

Usiku wa kuamkia Septemba 6 mwaka huu, kundi la vijana takriban 30 wahalifu wa mitaani, maarufu panya road lilivamia nyumba 15 na kujeruhi watu wanne na kupora fedha na mali katika mtaa huo tajwa.

Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Wiliam Mkonda, alisema juzi kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni ya kuzuia uhalifu maeneo mbalimbali.

Alisema kutokana na tukio hilo lililotokea saa 3:13 usiku wa siku hiyo, Jeshi la Polisi lilimkamata Selemani Kalembo (57), maarufu Sele Bonge, mkazi wa Vingunguti na wenzake tisa, wakiwa na gari lenye namba za usajili T 218 BYS aina ya Noah.

Alisema kuwa watu hao walikutwa wakiwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia, televisheni nne, kamba na mfuko wa kufichia viambaza (TV) baada ya kuiba.

“Mahojiano ya kina yanaendelea ili kuwakamata wote walioshirikiana nao. Jeshi la Polisi limeendelea na vikao na wananchi wa Kinyerezi na maeneo mengine ya jiji, vyenye lengo la kuimarisha na kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi, kwa maeneo ambayo hayana,” alisema.

Kamanda Mkonda aliwataka viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika mikakati ya kupeana elimu na kuhakikisha kila mtaa unakuwa navyo.

“Tunawaomba wananchi waendelee kushirikiana na polisi katika kutoa taarifa za kuwabaini wahalifu na linaahidi kutunza siri hizo.

“Tunaendelea na operesheni maalum maeneo yote na tunatoa onyo kwa mtu au kikundi kinachojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja,” alisema.