Bendera zilishushwa katika kumuombolezea Malkia, Elizabeth na ilipandishwa juu baada ya hafla hiyo kumalizika.
Hafla ya utanganzaji wa mfalme huyo mpya ilipeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni kwa mara ya kwanza.
Charles alipokea Ufalme baada ya kifo cha mama yake Malkia Elizabeth II, aliyefariki jumamosi.
Baraza la kumtangaza rasmi Mfalme, lilijumuisha wanasiasa wakuu, majaji na maofisa wengine ambao walimtangaza rasmi kama mfalme.
Ni mara ya kwanza hafla hii inapeperushwa kwenye televisheni.
Matangazo mengine yatatolewa rasmi nchini kote Uingereza mpaka Jumapili, wakati bendera zitarudi kupepea nusu mlingoti.
Haya yanajiri baada ya Mfalme Charles kuahidi kumfuata, kipenzi mama yake kujitolea maisha kuhudumia watu katika hotuba yake ya kwanza iliyojaa huzuni.
Siku ya Ijumaa ameliambia taifa lake jinsi alivyohuzunika kwa kumpoteza mama yake, akisifia mzaha, ukarimu wake na uwezo wake wa kuona wema kwa kila mtu.
Mfalme ameahidi kulitumikia taifa kwa uwajibikaji usiotetereka kama aliokuwa nao marehemu mama yake Malkia katika utawala wake wa miaka 70.
Baada ya tangazo hilo, Mfalme atatoa tangazo binafsi kuhusu kifo cha Malkia na kula kiapo kulihifadhi kanisa la Uskotchi ambalo kuna mgawanyiko wa sheria kati ya kanisa na serikali.
Miongoni mwa watakaohudhuria hafla hii ni mkewe Camilla, ambaye amepokea wadhifa wa Malkia, mwanamfalme mpya wa Wales, William.
Tangazo la kwanza lilitolewa katika roshani ya Friar Court ya kasri la Mt. James mjini London saa tano saa za huko, muda unaoambatana na mbwembwe za wapiga tarumbeta, milio ya bunduki zinazofyatuliwa kwa heshima katika bustani ya Hyde na katika Jumba refu maarufu la London Tower.
Licha ya kwamba sio sehemu ya shughuli hiyo rasmi ya kutangazwa mfalme, maneno "Malkia amefariki, Mflame aishi Maisha marefu" mara nyingi hutamkwa baada ya hapo.
Juzi Charles alikutana na umati wa watu waliopiga kelele kumtakia maisha mema wakati akisalimiana na umati uliokuwepo nje ya kasri la Buckingham.
Baada ya hapo alitoa hotuba kwenye televisheni akieleza matumaini kwamba Mwanawe William kama Mwanamfalme mpya wa Wales na mkewe Catherine wataendelea kuwatia watu moyo na kuongoza mdahalo wa kitaifa.
AFRIKA ITAMKUMBUKA MALKIA
Malkia Elizabeth II alikuwa na nafasi maalum moyoni mwake kwa ajili ya Afrika, alikuwa barani humo katika nyakati muhimu za maisha yake.
Akiwa Afrika, wakati huo alikuwa akiishi katika Hoteli ambayo sasa imefungwa ya Treetops nchini Kenya, baba yake Mfalme George wa Sita, alipofariki na akawa Malkia akiwa na umri wa miaka 25 pekee.
Wakati wa utawala wake wa miaka 70 alitembelea zaidi ya nchi 20 za Kiafrika, na aliwahi kusema kwa mzaha mbele ya Nelson Mandela aliyekuwa akitabasamu kwamba amekuwa Afrika zaidi kuliko mtu yeyote, na kusababisha vicheko vikali kutoka kwa wale walio karibu naye.
Malkia huyo alikuwa na uhusiano mzuri binafsi na Mandela ambaye alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini na kinara wa vita dhidi ya utawala wa wazungu wachache nchini humo.
Taasisi ya Mandela ilionyesha kusikitishwa kwake na kifo chake.
"Mandela na Elezabeth walizungumza kwenye simu mara kwa mara, wakitumia majina yao ya kwanza kama ishara ya kuheshimiana na vile vile upendo."
Taarifa hiyo ilisema alikuwa na jina maalum la Malkia, Motlalepula, ambalo linamaanisha Malkia wa mvua, kwa sababu ziara yake ya 1995 nchini humo wakati wa utawala wake iliambatana na mvua ya kumkaribisha.
Baada ya kurithi himaya kubwa iliyoenea katika bara la Afrika, baada ya kuwa Malkia enzi zake zilishuhudia makoloni yote 14 ya Waingereza katika Afrika yakipata uhuru wao, kuanzia na Ghana mnamo 1957.
Malkia aliweza kudumisha uhusiano wake na Afrika kwa kupitia uundaji wa Jumuiya ya Madola mwaka 1961, alipigwa picha akicheza na Kwame Nkrumah, ambaye aliongoza kampeni ya uhuru wa Ghana na kuwa rais wake wa kwanza.
Neno himaya liliachwa wakati wa kiapo chake cha kutawazwa mnamo 1953.
Viongozi kutoka barani kote Afrika wametoa salamu za pole kwa Uingereza
Rais wa nchi ya Kenya ambako safari yake kama Malkia ilianza, Uhuru Kenyatta, aliomboleza kifo chake akimtaja kama alama ya juu ya utumishi wa kujitolea kwa ubinadamu na kiongozi mkuu, sio tu Uingereza na Jumuiya ya Madola ambayo Kenya ni mwanachama mashuhuri lakini ulimwengu mzima.
Ingawa uhusiano kati ya Zimbabwe na Uingereza umekuwa sio mzuri kwa miaka mingi, jambo lililosababisha hayati Rais Robert Mugabe kujiondoa katika Jumuiya ya Madola, mrithi wake Emmerson Mnangagwa aliandika haraka kwenye Twitter kwamba anatoa pole ya dhati kwa Familia ya Kifalme na watu wa Uingereza, na Jumuiya ya Madola.
Kiongozi wa Nigeria, koloni kubwa zaidi la zamani la Uingereza barani Afrika, Muhammadu Buhari alimwandikia salamu za pole ndefu kwenye Twitter, akisema amepokea kifo chake kwa huzuni kubwa.
"Hadithi ya Nigeria ya sasa haitakamilika bila ukurasa wa Malkia Elizabeth ll, mtu mashuhuri duniani na kiongozi bora. Alijitolea maisha yake kufanya taifa lake, Jumuiya ya Madola na dunia nzima kuwa mahali pazuri."
Pia alimkaribisha mrithi wake Mfalme Charles III kwenye kiti cha enzi.
Rais Ali Bongo wa Gabon, ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa ambalo lilijiunga na jumuiya hiyo mwezi Juni, pia ametuma salamu zake za rambirambi.
Licha ya kumiminika kwa salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wa bara hilo, baadhi ya Waafrika wengine wamezungumzia mateso yao chini ya utawala wa Waingereza, wakieleza kuwa ukoloni ulifanywa kwa jina la familia ya kifalme.
Baadhi ya Falme zenyewe za Kiafrika pia wameelezea masikitiko yao.
Prince Mangosuthu Buthelezi alitoa heshima zake kwa niaba ya Mfalme Misuzulu KaZwelithini, kiongozi wa Wazulu wa Afrika Kusini.
Aliangazia urafiki wake wa kuthaminiwa na Mfalme Charles III, akimtumia salamu binafsi za rambirambi.
Mfalme Misuzulu yuko katika nafasi nzuri ya kuelewa kile ambacho Mfalme Charles anapitia, kwani baba yake mwenyewe, Zwelithini, alifariki mwaka jana, baada ya miaka 50 ya kiti cha enzi.
Malkia alikuwa kwenye ziara ya Afrika Kusini aliposherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 21 mwaka wa 1947.
Katika hotuba yake maarufu ya redio kutoka Cape Town, alijitolea maisha yake kwa Jumuiya ya Madola na kusema alijisikia nyumbani akiwa nchini Afrika Kusini kana kwamba alikuwa akiishi hapo maisha yake yote.
Akiwa maarufu duniani kote kwa uwezo wake wa kubaki kwenye siasa, alitoa kauli kali mwaka 1995, akizuru Afrika Kusini mwaka mmoja tu baada ya Mandela kuwa rais na kumaliza mfumo wa ubaguzi wa rangi uliohalalishwa unaojulikana kama ubaguzi wa rangi.
Aliipongeza nchi hiyo kwa maendeleo yake na kusema
"Mmekuwa taifa moja ambalo roho yake ya upatanisho ni mfano mzuri kwa ulimwengu, na nimerudi kujionea mwenyewe kile ambacho si muujiza mdogo."
BBC










