Alitoa hadi hiyo jana alipozungumza na wananchi katika Jimbo la Isimani wakati akihitimisha ziara yake mkoani Iringa.
"Serikali ina dhamira njema kwa wananchi wake. Ninajua bidhaa mbalimbali zimepanda bei na tunaendeleza mapambano ili kuleta unafuu. Kama tulivyofanya kwenye ruzuku ya mbolea, tutafanya hivyo na kwingine," aliahidi.
Rais Samia alitoa ahadi hiyo baada ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, kuzungumzia kupanda kwa bei ya bidhaa, zikiwamo sabuni.
Waziri huyo alisema bidhaa hiyo imepanda kutokana na kupungua kwa malighafi ambazo hutumika kuitengeneza, kwa kiasi kikubwa zikiagizwa nje ya nchi.
"Ndugu zangu, serikali inatambua changamoto mnazokutana nazo kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali na hii ni kutokana na baadhi ya nchi tunazozitegemea kupata malighafi, kufunga mipaka yake. Hata hivyo, tayari tumefanya mazungumzo nao, tayari wamefungua mipaka," waziri huyo alisema.
Waziri Kijaji alisema kwa sasa tayari mipaka imefunguliwa na baada ya miezi miwili, bei ya sabuni itashuka.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha inaleta unafuu kwa wananchi licha ya mabadiliko mbalimbali yanayoikumba dunia kwa sasa.
Mbunge wa Isimani, Wiliam Lukuvi, aliipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni huko, akitolea mfano miradi ya umwagiliaji.
ULINZI MAZINGIRA
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka Watanzania kulinda misitu kwa kuacha kukata miti ovyo kwa lengo la kupata kuni na mkaa.
Akiwa njiani kurejea Dodoma, Rais Samia alirejea ujumbe wake huo alioutoa mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe, kwa wakazi wa Kata ya Mpunguzi jijini Dodoma aliposimama kuwasalimia.
“Kwenye suala la mkaa nilikuwa ninaangalia kutoka Mtera hadi hapa ni mkaa njia nzima, misitu inateketezwa lakini habari nzuri ni kwamba Wizara ya Madini inakwenda kuzindua mkaa unaoitwa mkaa rafiki unaotokana na vumbi la makaa ya mawe, jiandaeni badala ya kukaa porini kukata miti, mtachukua mkaa huu na kwenda kuuza kwenye maeneo yenu ili misitu yetu inusurike," aliagiza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, aliwataka Watanzania kuendelea kutunza misitu na vyanzo vya maji ili kuzilinda rasilimali za taifa.
*Imeandikwa na Francis Godwin na Martha Sambo (IRINGA) na Paul Mabeja (DODOMA).










