DTB yazindua kampeni mpya kuimarisha huduma zake

24Oct 2022
Mary Kadoke
DAR ES SALAAM
Nipashe
DTB yazindua kampeni mpya kuimarisha huduma zake

BENKI ya Diamond Trust Bank (DTB) imezindua kampeni mpya inayoitwa Tuamini tukusogeze karibu na ndoto zako ‘Bank with us Bank on us’ katika mkakati wa kuimarisha utendaji wake pamoja na huduma kwa wateja.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DTB Tanzania Ravneet Chowdhury wa kwanza kushoto mstari wa tatu karibu na kibao akiwa na wafanyakazi wa benki hiyo baada ya kuzindua kampeni mpya inayoitwa Tuamini tukusogeze karibu na ndoto zako ‘Bank with us Bank on us’ wikiendi hii jijini Dar es Salaam

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DTB Tanzania Ravneet Chowdhury, alisema hayo katika kampeni iliyoshirikisha wafanyakazi wa makao makuu ya benki hiyo wikiendi hii jijini Dar es Salaam.

Alisema pamoja na kampeni hiyo kulenga kukuza uwajibikaji wa wafanyakazi lengo lingine ni kuhakikisha inaimarisha imani kwa wateja ili kukuza ustawi wa benki hiyo.

“Tunaposema Tuamini tukusogeze karibu na ndoto zako tunamaanisha nini? Tunalenga mteja atuamini. DTB tayari imejenga imani kubwa sokoni. Tuna wateja wazuri lakini pamoja na hayo, tunataka tuzidi kusonga mbele,” alisema.

Aidha alisema kwa jinsi teknolojia inavyozidi kukuwa siku hadi siku, benki hiyo inalazimika kuweka mikakati ya kuifanya izidi kusonga mbele.

“Nakutana na wateja wengi wanaoisifia DTB. Hauhitaji matangazo au mabango, kinachotakiwa ni kuwa na wateja wanaoridhika. Hivyo kwangu mimi kampeni hii ni muhimu kwani ni kama vile tunawaambia wateja tunarekebisha kila changamoto iliyopo na kuhakikisha kwamba kila kitu kinaenda sawa.”alisema.

Aliongeza: “Kwa wale wanaokutana na wateja tusipowasaidia kampeni zetu zitashindwa ni lazima tuhakikishe tunashirikiana ili kila kitu kiende sawa.”

Jesca Tugara, Naibu mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa benki ya DTB alisema kampeni hiyo imelenga kuwasogeza wateja karibu na ndoto zao, “Tunawaleta wateja karibu na ndoto zao kupitia huduma za kibenki au mikopo. Tunaweza tusikufikishe sehemu yenyewe lakini tunakuwa tumekusogeza karibu na ndoto zako kwa njia moja ama nyingine.”

Baadhi ya kampeni zilizowahi kutumika awali ni pamoja na ‘Faidika zaidi’ pamoja na ‘Benki Bora, Benki salama’.

Chowdhury alisema mkakati mpya katika usimamizi wa fedha umefikia lengo kwa mwaka huu na kufikia shilingi 1.3trn.