W'biashara wadogo wahukumiwa miaka 20 jela kusafirisha dawa za kulevya

15Feb 2023
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
W'biashara wadogo wahukumiwa miaka 20 jela kusafirisha dawa za kulevya

WAFANYABIASHARA wadogo wawili waliokuwa wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi katika Mkoa wa Manyara, wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja.

Wafanyabiashara hao walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Babati, kutumikia adhabu hiyo ni Swalehe Mohamed (27), mkazi wa Mdori, Wilaya ya Babati na Yahaya Bakari (37), mkazi wa Ngaramtoni, jijini Arusha.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Victor Kimario.

Kabla ya kusoma kwa hukumu hiyo, Hakimu Kimario, alisema mshtakiwa Swalehe Mohamed, ametiwa hatiani, baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kwamba, alikuwa mmiliki wa misokoto 125 ya bangi, sawa na gramu 450.

Alisema mshtakiwa Swalehe, alikutwa na misokoto hiyo Desemba 29 mwaka jana nyumbani kwake Mdori, akiwa amehifadhi chumbani.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, mshtakiwa alikiuka Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Kifungu cha 15A (1) (2) (C) ya Mwaka 2005 iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2019.

 

 

Aidha, mshtakiwa mwingine, Yahaya Bakari (37), Mkazi wa Ngaramtoni jijini Arusha, pia ametiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani, baada ya kuthibitika alikuwa akisafirisha mirungi bunda 247, sawa na kilogramu 94.85.

Mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya usafirishaji wa mirungi, Frank Mushi (45), mkazi wa Sakina jijini Arusha, yeye anaendelea na kesi hiyo baada ya kukana kuhusika kusafirisha dawa hizo.

Hakimu Kimario, wakati anasoma hukumu, alisema washtakiwa hao walikamatwa Februari 2, mwaka huu katika Kijiji cha Bonga, Wilaya ya Babati, wakiwa wanasafirisha mirungi, kwa kutumia gari lenye namba za usajili T.686AHW aina ya Fuso, mali ya Kampuni ya Kisare.