Walimu walevi waonywa

12Sep 2023
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Walimu walevi waonywa

WALIMU wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, wametakiwa kuzingatia maadili na kuepukana na matumizi ya dawa ya kulevya, unywaji wa pombe kupindukia katika kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuboresha taaluma na ufaulu kwa wanafunzi.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Morogoro,Mbaruku Ligubi Chipeta.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Morogoro,Mbaruku Ligubi Chipeta wakati akizungumza na walimu wa ajira mpya waliopangiwa vituo vya kazi katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo.

Chipeta amesema kuwa mwalimu ni kioo kwa jamii inayomzunguka ambapo maadili yake yanatoa taswira chanya kwa wanafunzi anaowakufundisha na kwa kuwa haiba yake inamwongezea ari mwanafunzi kufuata nyayo na maadili mema kwa maisha yake kielimu na kijamii.

Amesema kuwa chama cha walimu kina jukumu la kuwatetea walimu kote nchini kwa kuweka mshikamano kwa kuzingatia kauli mbio yao wajibu na haki,hivyo mwalimu anapotimiza wajibu wake anapaswa kutetewa kupata haki yake ikiwemo masilahi na kulipwa stahiki zake kwa wakati.

“Niwaombe walimu wenzangu mliopata ajira hii mpya,mkalete chachu kwenye kuleta mapinduzi ya kuboresha elimu kwa kuwa hali ya ufaulu kwa shule zetu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni siyo ya kuridhisha,hivyo tushirikiane katika kuboresha ufaulu katika shule zetu.”alisema mwenyekiti huyo.

Ametoa rai kwa walimu kuepukana na kuchukua mikopo kwenye taasisi zisizo na rasmi na badala yake watumie taasisi rasmi za fedha ikiwemo kwenye benki ambako ni salama zaidi.

Naye, Afisa utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro,B’hango Lyangwa amewataka walimu hao kuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan katika utendaji kazi kwa uweledi ili kuleta ufanisi kwenye sekta ya elimu.

Lyangwa amesema kuwa jukumu la walimu kote nchini ni kuhakikisha ya kuwa taifa linaondokana na adui ujinga,hivyo utendaji wa kazi wa mwalimu ndio unaofinyanga wanajamii kwa kutoa maarifa mbalimbali yanayosaidia kulijenga taifa.

Afisa utumishi huyo aliwakumbusha walimu hao kutojihusisha na makundi yasiyo kuwa na maadili watakayokutana nayo katika jamii.