Washindi shindano la ma-DJ hawa hapa

08Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Washindi shindano la ma-DJ hawa hapa

HATIMAYE bia pendwa ya Serengeti Lite, imehitimisha shindano lake la 'DJs' lililopewa jina la 'Take a Bite Out of Life' kwa kuwatunuku ma-DJ watatu bora nchini vifaa vya kupigia muziki vyenye thamani ya Sh. milioni saba kila mmoja, tukio hilo likifanyika Ukumbi wa Triple-A Arusha.

Tukio hilo lilihitimisha kampeni ya miezi mitatu kwa kupata ma-DJ watatu kutoka kanda saba nchini. Pia washindi hao wamepata fursa adimu za kuwa ma-DJ rasmi wa chapa ya Serengeti Lite katika promosheni na shughuli zake za utangazaji nchini.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Bia cha SBL, Nandy Mwiyombella, kwanza aliwapongeza washindi hao; Abduliazizi Juma 'Dully TZ' kutoka Dodoma, aliyeshika nafasi ya kwanza, Steven Jonathan 'DJ Stegio wa Dar es Salaam na Mussa Shaban 'DJ Son' kutoka Kilimanjaro.

Alisema: "'Ni wakati wa kusisimua kwa SBL na bia yake ya kipekee, Serengeti Lite, ambayo imetumia shindano hili ili kuwasaidia vijana kuonyesha vipaji vyao. Serengeti Lite ina shauku ya kuwaona vijana wakionyesha umahiri wao katika vipaji walivyonavyo.

"Vilevile shabaha ya 'Take a Bite Out of Life', ililenga kutoa burudani kwa wateja wetu katika maeneo waliyopo ili waendelee kufurahia kinywaji chenye ladha kamili cha Serengeti Lite, Bia ya Kitanzania iliyotengenezwa kwa ajili ya Watanzania na ya Watanzania."

Ofisa Vijana wa Arusha, Japhet Kurwa, ndiye aliyeongoza hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, John Mongella, ambaye pia aliwatunuku washindi watatu waliobahatika huku akipongeza juhudi za SBL za kuchochea soko la ajira kwa kutoa motisha kwa vijana kupitia sekta ya burudani.

"Nimejawa na furaha kubwa sana baada ya kushuhudia jinsi vijana wanavyopambania ndoto zao kwa nguvu na ari. Nawapongeza sana SBL kwa kutimiza ndoto zao, ni siku nzuri kwa washindi hawa watatu; maisha yao hayatakuwa sawa tena kwa sababu fursa hii imekuwa chanzo cha ajira kwao. Nina uhakika pia kuwa washiriki wengine (hasa washindi) mtaanza kupokea mialiko mingi kwenye hafla za kutumbuiza muziki maeneo mbalimbali na pengine kufungua studio zenu za muziki hapo baadaye.

"Tukio la leo limekuwa gumzo na kuibua hisia nzuri sana kwa vijana hapa Arusha. Ni matumaini yetu kama serikali ya mkoa, kuwa vijana wamehamasika kujiinua kimaisha na kuchangamkia kila fursa zingine zilizopo ili kufikia malengo yao hasa katika hiki kipindi ambacho serikali yetu inafanya kazi kubwa ya kuongeza ajira nchini," alisema Kurwa.

Kampeni ya Take a Bite Out of Life iliambatana na shughuli za burudani kutoka kwa ma-DJs wa ndani walioshindana katika wilaya na mikoa nchini kote ambapo shindano hilo lilishirikisha zaidi ya washindani 5,200 wenye zaidi ya miaka 18 na matarajio ya kujenga vipaji vyao kama waburudishaji wa muziki.

Hii si mara ya kwanza kwa SBL kuwekeza katika miradi kama hii. SBL pia imewekeza katika sekta ya michezo kwa kudhamini timu ya Taifa Stars, Ligi ya Taifa ya Wanawake na mashindano mengine muhimu ya gofu.