Odemba: Nimeishia darasa la saba lakini naitangaza nchi yangu vizuri

28Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Odemba: Nimeishia darasa la saba lakini naitangaza nchi yangu vizuri

MWANAMITINDO na mmiliki wa Odemba Foundation, Miriam Odemba amemwaga machozi mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo wakati akielezea historia ya maisha yake jinsi alivyokosa elimu na kuishia darasa la saba.

MWANAMITINDO na mmiliki wa Odemba Foundation, Miriam Odemba.

Tukio hilo limetokea jana wakati Odemba alipoenda wilayani humo kutoa misaada kwa wanafunzi wa shule za kisarawe katika kuchangia kampeni ya tokomeza zero iliyoanzishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Jokate Mwegelo. 

Odemba alianza kwa kusema kuwa kitu ambacho alikikosa katika maisha yake ni elimu ingawa alijiendeleza kielimu baadae. 

“Siwezi kuficha nimeishia darasa la saba lakini nimejiendeleza sana kielimu pia ni 'model' kama mnavyoniona nina kipaji Mwenyezi Mungu amenipa kipaji cha kuweza kuwa mimi, mpaka sasa hivi hata kama elimu ya shule nilikuwa sina lakini nina kipaji kingine naitangaza nchi yangu vizuri huko nchi za nje," amesema Odemba

Baada ya historia hiyo Mkuu wa wilaya hiyo (Jokate) alishindwa kujizuia na kujikuta akimwaga machozi.

Akielezea jinsi alivyoguswa, DC Jokate, amesema kuna mapito mbalimbali ambayo watu wengi wanapitia."Kuna kipindi mama yangu alikuwa anajinyima sana kuna vitu yeye afanyi ili tu apate hela ya kutusomesha shule nzuri ili tupate elimu nzuri, kwa hiyo amenigusa sana (Odemba) kwa sababu naelewa na natambua ni jinsi gani wazazi wetu walijitoa sana ili sisi tuweze kufanikiwa," amesema Dc Jokate 

Imeandikwa na Adelina Charles, TUDARCo