Nay wa Mitego: Naipeleka Basata mahakamani

24Jul 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Nay wa Mitego: Naipeleka Basata mahakamani

BAADA ya kufungiwa wimbo wake wa 'Pale Kati Patamu', rapa Nay wa Mitego amesema hatua hiyo imemuumiza kutokana na kile alichodai kwamba ametumia gharama kubwa hadi kuutoa.

Nay wa Mitego

Alisema kuwa anaendelea kuwasiliana na wanasheria wake ili kuangalia uwezakano wa kuchukua hatua zaidi ambazo zitaufanya wimbo huo ufunguliwe na kuanza kusikika kama kawaida.

Alisema kuwa hakutarajia kwamba utafungiwa, kwa madai kwamba hakuna maneno makali ya kusababisha zichukuliwe hatua kama hizo, hivyo ameona kuna haja ya kufuatia haki yake.

"Mimi ninashangaa kwa nini nyimbo ambazo zinaashiria matusi ukiwamo wa Muhogo wa Jang'ombe na nyingine nyingi hazijawahi kufungiwa, lakini ninaonewa mie tu na sasa ni wimbo wa tatu kufungiwa," alisema huku akisema mwanasheria wake ataangalia kama waende mahakamani.

Wiki iliyopita Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) lilifungia wimbo huo ikiwa ni miezi michache tangu lifanye hivyo katika wimbo mwingine wa msanii huyo uitwao 'Shika Adabu Yako'.