Bunge lajadili nyimbo  za wasanii kufungiwa 

11Apr 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Bunge lajadili nyimbo  za wasanii kufungiwa 

SAKATA la kufungia nyimbo za wasanii nchini jana limetinga bungeni huku serikali ikisisitiza kuendelea kuzifungia nyimbo ambazo zinakiuka maudhui na maadili huku ikifafanua kuwa hatua hiyo sio vita kwa wasanii.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Aidha, imesema hata mataifa mbalimbali yamekuwa yakifungia nyimbo za wasanii wao huku Shirika la Utangazaji nchini Uingereza (BBC) likifungia nyimbo 237 katika historia yao.

Hayo yalibainishwa jana bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Magige.

Katika swali lake, Magige alisema pamoja na kuwapo na kamati ya maudhui, lakini wasanii wamekuwa wakifungiwa nyimbo zao wakati wametafuta fedha za kurekodi kwa shida hasa ikizingatiwa kuna uhaba wa ajira.

“Waziri anaweza kutuambia kamati hii ya maudhui imeshindwa kazi kwa sababu wamekuwa wakiacha hadi nyimbo zinatoka ndo wanakuja kufungia wasanii wetu,”alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Mwakyembe alisema kila taifa lina utamaduni wake na lazima ulindwe kwa udi na uvumba.

“Tunachokifanya sio kwamba tuna vita na wasanii wetu bali ni kulinda maadili katika kipindi hichi cha utandawazi na maendeleo ya kasi ya teknolojia ya habari kuna mmomonyoko wa maadili ya nchi yetu, lazima tuchukue hatua.

“Kinachofanyika hapa sio cha pekee duniani kila mtu anafanya hivyo, hawa wasanii wetu tumeshawasamehe wasirudie tena,”alisema.

Aliongeza kuwa mwanamuziki Rick Ross wa Marekani, ambaye ameimba pamoja na nyota wa muziki Daimond Platnumz wimbo wa ‘wakawaka’, amepata matatizo Marekani kwa kuimba wimbo wenye maudhui ya kuunga mkono vitendo vya ubakaji.

“Marekani nzima wakina mama walikuja juu wimbo ukaondolewa kwenye television zote, lakini yule kijana akaomba radhi kwa wanawake wote, sasa kwa Tanzania sisi tumekuwa kokoro tupokee kila kitu kwa sababu hatuna utamaduni,”alisema.

Alisema mwanamuziki maarufu duniani kutoka nchini Nigeria, Davido ambaye pia kaimba na Daimond amefungiwa nyimbo zake mbili mwaka huu.

“Wizkid kafungiwa nyimbo zake sijaona wabunge wa Nigeria wakilalamikia sheria zao wenyewe, sisi wabunge kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunalinda na kuheshimu sheria za nchini na tutaendelea kuzifungia,”alisisitiza.

Alisema msanii Koffi Olomide amefungiwa wimbo wake wa 'Ekotikee' na ni marufuku kupigwa Kongo kwa kuwa ni wimbo wa matusi.