Wavuvi, wananchi wapewa angalizo uhifadhi viumbe baharini

11Mar 2024
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Wavuvi, wananchi wapewa angalizo uhifadhi viumbe baharini

MENEJA wa Hifadhi ya Kisiwa cha Mnemba (MIMCA), Yassir Ali Haji, kutoka Idara ya Uhifadhi wa Bahari amewataka wavuvi na wananchi kufuata sheria zilizowekwa na mamlaka zinazohusika na uhifadhi wa viumbe wa baharini ikiwemo kiumbe cha baharini (pomboo), ili kuepusha na athari zinazoweza-

pomboo.

-kujitokeza kwa viumbe hao.

Akitoa elimu jinsi ya kuangalia pomboo wanapokuwa baharini kwa wadau wa sekta ya utalii, wananchi na wavuvi huko Nungwi na Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja jana.

Amesema viumbe hao wako hatarini kutoweka kwenye hifadhi kutokana na kujitokeza kwa wadau wa utalii na wavuvi kutofuata sheria wakati wanapokwenda maeneo hayo kuangalia pomboo.

Amesema viumbe hao wanahitaji utulivu na hawapendi kelele, hivyo ipo haja kwa wadau hao kufuata sheria ili kuepusha pomboo kukimbilia maeneo mengine.

Aidha amesema viumbe hao ni muhimu kuwepo sehemu za kihistoria na hifadhi kutokana na kuwa kivutio kikubwa cha watalii.

“Viumbe hawa wamekuwa na tabia ya woga wanapokuwa baharini na pia hawapendi kusikia kelele wakati wanapokuwa baharini jambo la msingi kwa wadau wanaokwenda kuangalia viumbe kufuata sheria”, amesema.

Pia aliwataka wavuvi kuacha kutupa nanga maeneo hayo ya hifadhi kuepuka kuharibu matumbawe na rasilimali nyingine za baharini.

Ofisa Mazingira ya Bahari, Thuwaiba Kassim Haji kutoka Idara ya Uhifadhi wa Bahari amewataka wadau kusoma tabia za pomboo ili kuepuka kuwaondoa katika makazi yao jambo ambalo linaleta shida kwa viumbe hao.

Ofisa kutoka Kamisheni ya Utalii Ame Nassor Juma, amesema Pomboo ni muhimu kuwepo katika maeneo ya historia na hifadhi za bahari kutokana na fursa ya ajira kwa wananchi wa Zanzibar na kuongeza pato la serikali kupitia utalii.

Wakitoa maoni yao wadau wa sekta ya utalii wameitaka Idara ya Uhifadhi wa Bahari kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau wa utalii na wavuvi juu ya umuhimu wa kuhifdhi pomboo kwa kuwa ni miongoni mwa kivutio kikubwa cha watalii.

Juma Makame Sheha ambae anajishuhulisha na kuwatembeza watalii baharini amesema wapo wavuvi ambao hukokota nyavu sehemu za hifadhi na kusababisha kunasa kwa pomboo kitu ambacho siyo kizuri kufanyika katika hifadhi ya bahari.

Hivyo, ameitaka serikali kuweka boti maalum za kufuatilia pomboo wanaokimbilia baharini kuimarisha sekta ya utalii.