SELF yaandaa mwarobaini wa mikopo umuza kwa wananchi

12Mar 2024
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
SELF yaandaa mwarobaini wa mikopo umuza kwa wananchi

MFUKO wa Fedha wa SELF umesema unaendelea kutanua wigo wa utoaji mikopo nchini ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi, kwa ajili ya kuwaepusha na wakopeshaji binafsi wanaowakopesha kwa masharti magumu maarufu kama kaushadamu au mikopo umiza.

MFUKO wa Fedha wa SELF umesema unaendelea kutanua wigo wa utoaji mikopo nchini ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi, kwa ajili ya kuwaepusha na wakopeshaji binafsi wanaowakopesha kwa masharti magumu maarufu kama kaushadamu au mikopo umiza.

Mfuko huo unaomilikiwa na serikali unajihusisha na utoaji mikopo kwa wafanyabiashara wa chini na kati, unajivunia kuwafikia zaidi ya wakopaji 300,000 katika matawi 12 nchini.

Mtendaji Mkuu wa Taaasisi hiyo ya kiserikali, Mudith Cheyo, ameyasema hayo wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu utekelezaji wa shughuli zao kwa miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kwa sasa wananchi wengi wanakwenda kwenye mikopo binafsi yenye majina mengi (mikopo umuza, kausha damu) ambayo ina masharti magumu, na kwamba wamejipanga vyema kuhakikisha wanakuwa kimbilio kwa wahitaji.

Cheyo amesema taasisi hizo zimekuwa zikitoa mikopo kwa wafanyabiashara kwa masharti magumu bila ya kuwachunguza uwezo wao na kuwapa elimu ya ujasiriamali, hali inayowapelekea kushindwa kulipa deni kwa wakati na kuwafilisi.

Amesema mfuko huo kabla ya kumpa mteja mkopo wanatumia muda kumchunguza na kumjua zaidi kwa kuangalia mambo mbalimbali ikiwamo nia yake ya kutaka mkopo, uwezo wa kuendesha biashara anayoichukulia mkopo, wanahitaji kujengewa uwezo gani ili afikie malengo yake na alipe rejesho kwa wakati.

Amesema kwa takribani nane waliotoa huduma hiyo, wamegundua kuwa baadhi ya wanakwenda kukopa hawana elimu ya fedha, wanaendesha biashara zisizo rasmi na wengine hawana utamaduni wa kukopa hali inayopelekea kuchukua pesa na kufanyia mambo yao binafsi badala ya lengo kusudiwa.

Kwa mujibu wa Cheyo, wanakabiliana na hali hiyo kwa kuwapa elimu ya fedha ya na kumwongoza katika biashara yake ili kuhakikisha fedha alizochukua wapeleke kwenye malengo kusudiwa.

"Wakati mwingine tunagundua kuwa mteja wala haitaji mkopo bali anahitaji msaada na usimamizi wa kuendesha biashara aliyonayo kwa mtaji alionao, kwa hiyo tunampatia anachohitaji," amesema.

Mkurugenzi wa Biashara, Petro Mataba amesema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2015 na kupewa ruzuku na Sh.bilioni 56 na serikali na sasa wamefikisha Sh. bilioni 62 na sasa wanalipa gawio la zaidi ya Sh. milioni 200 kwa serikali, mwaka ulioishia 2023 walipata faida ya Sh. bilioni 2.

Amesema hadi kufikia Decemba, 2023 mfuko ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Sh. 324,506,402,014, ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu chini ya 10% na kuzifia taasisi binafsi 314,055 kati ya milioni 4 zinazohitaji kupata huduma hizo.

"Kati yao wanawake 166,449 sawa na asilimia 53 na wanaume 147,606 sawa na asimia 47. Wanufaika hao wanatoka katika mikoa 30 ya Tanzania Bara na Visiwani."

Mkurugenzi wa Masoko, Santiel Yona, amesema, ndoto ya mfuko huo ni kwa miaka 25 ijayo kuwa na matawi katika mikoa yote nchini Tanzania, ili kuwafikia wafanyabiashara wengi hasa wadogo ambao huishia kufilisiwa kwa kukopa sehemu zisizoendana na uwezo wao.

Ameitaja maeneo ambayo wameifikia mpaka sasa kuwa ni Dar es Salaam, Zanzibar, Morogoro, Shinyanga, Tabora, Katavi, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Geita, Kagera, Kigoma, Mtwara, Lindi, Tanga, Mwanza,Simiyu, Mara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Dodoma , Singida, Mbeya, Songwe na Rukwa.