Mkuu wa Wilaya ya Chato, mkoani Geita, Mhandisi Deusdedith Katwale, ameyasema hayo wakati akiongea na watumishi.
“Unakuta Mhandisi anakwenda kivyake, ofisa manunuzi kivyake na wakuu wa idara zinazotekeleza miradi husika nao kivyao, kwa staili hiyo hatuwezi kufika hata kidogo badala yake mnapaswa kushirikiana, kusaidiana na kukosoana kwa staha,” amesema Katwale.
Amesema inasikitisha kuona miradi inatekelezwa chini ya kiwango kutokana na baadhi ya wakuu wa idara kutoelewana huku akiwasihi kufanya kazi kwa uwazi, ukweli na uzalendo kwa manufaa mapana ya jamii badala ya kulenga kutaka kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa siku 90 kwa maofisa afya kata, watendaji kata pamoja na vijiji na maofisa tarafa kusimamia utekelezaji wa usafi wa mazingira, kwa kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na kusisitiza kuwa, agizo hilo ni amri wala siyo hiari.
“Atakayekaidi sheria ichukue mkondo wake, haiwezekani kwa karne hii watu kuendelea kuhimizwa kujenga vyoo, ni muhimu kuzingatia afya ya jamii ili kuepuka magonjwa mbalimbali,” amesema Katwale.
Ofisa Afya Wilaya hiyo, Fransisca Charles, amekiri kuwapo kwa baadhi ya kaya ambazo hazina vyoo na kwamba, mkakati umewekwa kuhakikisha kaya zote zinafikiwa na kuelimishwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matangi ya maji kwenye baadhi ya shule za msingi.
Amesema wilaya hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maofisa afya kata na kwamba, waliopo ni saba kati ya 23 wanaotakiwa.