Kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Kinondoni, Philipo Mwakibete, amepiga marufuku biashara hizo kufanyika katika masoko yote kwenye mamlaka hiyo ya serikali za mitaa.
Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa, Mwakibete amekemea vikali kitendo hicho na kuwataka wanaojihusisha na biashara hizo kuacha mara moja na katika Soko la Mwenge Coca Cola, kuanzia siku hiyo.
“Amri unatakiwa kuondoa biashara yako ya kamali, dubwi korokoro, pombe na dawa za kulevya katika eneo la soko la Mwenge Coca Cola kuanzia leo (juzi). Hutakiwi kuonekana katika eneo hilo kwa biashara hizi. Tafadhali upatapo barua zingatia agizo hili,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Waandishi wa habari hii walipomtafuta kwa ufafanuzi zaidi, Mwakibete alisema serikali imefikia uamuzi huo baada ya kupenyezewa taarifa na raia wema kwamba wako wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hizo.
Amesema biashara hizo ni kinyume cha sheria na miongozo ya masoko, hivyo wameamua kuwaandikia barua ya kuwataka kuacha mara moja.
Mwakibete amekumbusha kuwa maeneo ya soko ni sehemu jumuishi ambayo yanapokea kila aina ya watu na rika tofauti, hivyo uuzaji wa pombe, dawa za kulevya na kamali havileti sifa nzuri kwa wateja hasa watoto.
“Kwa mfano hapo sokoni tumejenga vyoo vizuri, lakini mtu akilewa anaenda kujisaidia haja ndogo inakuwa kero kwa mtu asiyetumia kilevi,” amesema.
Mwakibete amesema kwa wale watakaokaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwamo kuwabomolea mabanda na kutumia mamlaka nyingine za kiserikali ikiwamo polisi.
“Ndiyo maana ukiangalia hizo barua zimeenda kwa jina zimewalenga wahusika wanaojihusisha na hizo biashara na kama tutadili, tutadili na mtu kwa jina kwamba siku fulani tulikupa barua umekaidi agizo letu hapo ndipo tutakapoanzia, ukiacha na soko la Mwenge pia, la Msasani wanajihusisha na biashara hii,” amesema Mwakibete.
Vilevile amewataka wafanyabiashara kutoweka biashara ambazo haziruhusiwi kwenye masoko ana kuzingatia sheria.
Mwenyekiti wa Soko la Mwenge, Abdalah Samata, amesema biashara hizo si rafiki kwa ustawi wa soko hilo akiiomba serikali kutilia mkazo.
“Watumiaji wa bangi na pombe wakishalewa wanageuka wanaanza kuleta vurugu, kusumbua wateja na wakati mwingine wanachafua vyoo vya soko kwa kujisaidia ovyo.
Baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo wakizungumza na Nipashe wamesema wanakubaliana na uamuzi huo.
Mfanyabiashara Yassin Juma alisema anakubaliana na uamuzi wa serikali kuzuia kamali na dawa za kulevya na kutaka suala la pombe liangaliwe.
“Kama pombe imezuiliwa kwenye soko hili basi iwe nchi nzima na iwe inapatikana katika baa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa sababu siku hizi zinapatikana hata kwenye maduka ya mitaani ambako watoto wako,” amesema.
“Unakuta mtu anategemea hiyo biashara (pombe) kulea familia na pia wanarudishwa nyuma kiuchumi, sikubaliani na hatua hiyo, ninaunga mkono suala la bangi na kamali,” amesema Ally Kiumbe.
Mfanyabiashara mwingine, Martha Mosses, ambaye ni miongoni mwa waliopewa barua za kusitisha biashara ya pombe alisema ametii agizo hilo.
“Hatukuwahi kuitwa katika kikao ili tutoe maoni kuhusiana na suala hili, hata viongozi wa vinywaji wakiitwa kwenye vikao huwa hawapewi nafasi ya kuongea hata kidogo, ndio maana tumekubali walivyotaka wao sawa,” amesema.
* Imeandikwa na Halfani Chusi na Joyce Lameck










