Akizungumza jana wakati wa mkutano wa wadau wa kutoa maoni kuhusu rasimu ya mkataba wa huduma kwa wateja, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Mhina, alisema mkataba huo ni muhimu kwakuwa unawasaidia kwenye kujiendesha kiweledi.
“Uadilifu weledi na uwajibikaji tunatakiwa kwenda katika misingi ambayo inazingatia kanuni za utumishi wa uuma. Kwenye eneo la weledi ni lazima kuwe na viwango vya huduma bora kama taasisi ndipo pale tunapopambanua kuwafikia wateja wetu kila kundi lina matarajio yake," alisema.
“Ukiwa shambani kwako tunakuhudumia kwa huduma za ugani tunahakikisha tunakufikishia kwa wakati na kwenye mifugo hivyo hivyo. Hata kwenye masoko tunafanya hivyo hivyo pamoja na huduma za vibali haya yote yanagusa katika weledi.
Alisema wana matarajio makubwa watafikia malengo ya kutoa huduma bora ambazo zitaleta mabadiliko makubwa.
“Ninaamini tutafikia viwango na huduma zitaweza kuwafikia watu wengi tunafanya mapitio ya mkataba ulioandaliwa tangu mwaka 2014 hivyo kuna mabadiliko mengi ambayo yametokea. Kuna mabadiliko ya kiteknolojia tulikuwa katika analogy lakini sasa hivi tunatoa vibali kwa kutumia TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano),” alisema.
Ofisa Tawala Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wamoja Ayubu, ambaye ni mratibu wa rasimu ya mkataba kwa mteja, alisema mkataba huo unaelezea namna ambavyo mteja anaweza kurejesha mrejesho wa huduma ambayo amepata.
“Mchakato huu ulianza tangu Machi. Katibu Mkuu aliunda timu ambayo ilikaa na kupitia na tulitoka na rasimu na Mei iliwasilishwa kwenye wizara na mapendekezo yalitolewa sasa rasimu tumekuja kuwasilisha kwa wadau," alisema.
Alisema mkataba huo ni muhimu kwani unapima utendaji wa taasisi ambapo wateja wataweza kuwapima kama wanafikia vile viwango.
Naye, Ofisa Uhusiano na Masoko kutoka Kampuni ya Kilimanjaro International Leather Industries (KLIC), Fredrick Njoka, alisema wamehudhuria mkutano huo kama wanufaikaji na wanataka kuhakikisha wizara inakuwa na mikakati ambayo inawanufaisha wao.
“Zile changamoto ambazo tulikuwa tunaziona tunazitoa hapa hili ni jambo shirikishi na muhimu na hii ndio sehemu pekee ya kuelezea kuna vitu vingi ambavyo tunataka viongezeke,” alisema.










