Kampuni mpya yaanza kununua tumbaku

04Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kampuni mpya yaanza kununua tumbaku

SERIKALI imesema Kampuni ya Amy Holdings Limited imeanza ununuzi wa tumbaku na inataraji kununua tani 10,000 kwa msimu wa 2022/23.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, alibainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani.

Katika swali lake, mbunge huyo alihoji lini serikali itakamilisha majadiliano na kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco ili kurudi nchini kuendelea kununua tumbaku.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Mavunde alisema tumbaku hiyo itakayonunuliwa itachakatwa kwenye kiwanda kilichoko Morogoro ifikapo Julai, mwaka huu.

“Niwataarifu wakulima wa tumbaku nchini kuwa mwekezaji mpya ambaye ni mzawa kampuni ya Amy Holdings Limited amekamilisha taratibu za kuchukua shughuli zilizokuwa zinafanywa na Kampuni ya TLTC na ameshapewa leseni,” alisema.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya wawekezaji ambayo matokeo yake ni pamoja na kupatikana kwa mwekezaji huyo.

“Serikali itaendelea kufungua milango ya wawekezaji kuja nchini kuwekeza kwenye zao la tumbaku na itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha zao hili la tumbaku ili kupata wawekezaji na tumbaku ya wakulima inunuliwe,”alisema.

Hata hivyo, alisema wizara imetoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku kukaa na wadau wote kuangalia namna bora ya uendeshaji wa biashara ya tumbaku ili wakulima wanufaike na tumbaku yao.

Kuhusu wakulima wanaodai kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco, alikiri kuwapo kwa madai na kwamba Waziri (Hussein Bashe) alishawaita na kuwapa mwongozo wa malipo.

Alisema wamepewa hawatahuwisha leseni zao hadi pale watakapolipa madai ya wakulima.