Wakulima wa korosho kulipwa mabilioni

09Jan 2024
Na Mwandishi Wetu
TUNDURU
Nipashe
Wakulima wa korosho kulipwa mabilioni

WAKULIMA wa korosho katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma (TAMCU), wamevuka lengo la uzalishaji wa zao hilo katika msimu wa kilimo 2023/24.

Ni baada ya kufanikiwa kuzalisha na kuuza jumla ya tani 26,066 zenye thamani ya Sh. bilioni 45.531. Hilo ni ongezeko la tani 1,000 kulinganisha na msimu uliopita ambao walizalisha tani 25,000.

Kaimu Meneja wa TAMCU, Marcelino Mrope, alibainisha hayo jana alipozungumza na wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Ligunga (Ligunga Amcos) katika mnada wa nane na wa mwisho katika msimu wa kilimo wa 2023/24.

Mrope alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa wakulima na chama hicho katika uzalishaji korosho, akiwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya mashambani kwa mwaka 2023/24.

Alishukuru serikali kwa kutoa pembejeo za kilimo bila malipo kwa wakulima, hali iliyohamasisha wakulima wengi kurudi mashambani kwa ajili ya kufufua mashamba yao.

"Kwa mfano, katika msimu huu wa kilimo tumepewa pembejeo zenye thamani ya Sh. bilioni 22.5, kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu nchi ipate Uhuru. Tunaamini pembejeo hizi zitakwenda kuongeza sana uzalishaji korosho katika wilaya yetu," alisema Mrope.

Aliwashauri wakulima kutumia vizuri fedha walizopata kununua pembejeo na kutumia mvua iliyoanza kunyesha kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo.

Mwenyekiti wa TAMCU, Mussa Manjaule alisema bei ya korosho msimu wa mwaka huu haikuwa nzuri kulinganisha na msimu uliopita, lakini akawataka wakulima kutokatishwa tamaa badala yake waendelee kulima zao hilo ambalo ni nguzo kuu ya uchumi wao na Wilaya  ya Tunduru.

Manjaule alitoa ushauri kwa wakulima kuanza kulima mazao mengine ya chakula na biashara ikiwamo mbaazi zenye soko la uhakika na bei kubwa na halihitaji gharama kubwa katika uzalishaji wake.

Ofisa Ushirika wa wilaya hiyo, George Bissan, alipongeza Bodi ya TAMCU kwa kusimamia vyema mauzo ya korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umewezesha wakulima kuwa na soko la uhakika na kupata fedha zao kwa wakati.

Aliwaasa wakulima kutumia fedha walizopata kufanya mambo ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa nyumba bora, kusomesha watoto na kuanzisha shughuli nyingine zitakazowaingizia kipato badala ya kutumia fedha hizo kwenye ulevi na uwasherati.

Rashid Millanzi, mkulima wa korosho, aliipongeza serikali kupitia TAMCU kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Hata hivyo, mkulima huyo aliomba kutafuta wafanyabiasha wengi watakaokwenda kununua korosho kwa bei nzuri inayolingana na gharama za uzalishaji wake.