Hayo yamebainishwa juzi na Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU 2018 LTD), Samweli Jokeya.Alisema makisio hayo kuwa yanatokana na wakulima wanaotokana na vyama vya msingi vyenye wanachama 253.
Meneja Jokeya alitaja vyama hivyo vitakavyozalisha makisio ya msimu wa 2023/2023 ambayo ni kuanzia kilo milioni 42 hadi 54 kuwa vinatoka wilaya za Tabora, Uyui, Nzega na Sikonge.
Akizungumzia kuhusu pembejeo meneja huyo alisema hadi sasa asilimia 80 ya wakulima wamepata mbolea kwa ajili ya uzalishaji wa tumbaku kwa msimu ujao wa kilimo.
Aidha alitaja ongezeko la mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi kuwa miongoni mwa changamoto zinazokikabili kilimo hicho, huku zikiathiri suala la uwekaji wa mbolea shambani.
“Chama Kikuu cha Ushirika Kanda ya Magharibi tumeendelea kutoa elimu kwa wanachama wetu na kusisitiza wakulima wazingatie kilimo cha mazao ya chakula ili kujitosheleza kwa mahitaji pindi wanapokuwa wanavuna tumbaku na mazao mbadala kama tulivyowapa elimu na kuwaelekeza”alisema Jokeya.
Vilevile alitoa wito kwa wakulima hao wawe na kilimo cha zao mbadala tofauti na tumbaku, ili kuwa na uhakika wa chakula pamoja na biashara na kuacha kutegemea zao hilo kwa asilimia zote.









