Tigo kupeleka watu fainali za Afcon

28Dec 2023
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tigo kupeleka watu fainali za Afcon

KAMPUNI ya Tigo imezindua kampeni maalum ya 'Soka la Afrika Limeitika' yenye lengo la kuwapa fursa wateja wake kwenda kushuhudia fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Januari mwakani nchini Ivory Coast.

Fainali hizo za Afrika zimepangwa kuanza Januari 13 na kumalizika Februari 11 huku Tanzania ikishiriki kwa mara ya tatu fainali hizo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Huduma ya ongezeko la thamani wa kampuni hiyo, Adam Francis, alisema wateja wa kampuni hiyo wanaweza kujishindia zawadi mbalimbali ikiwamo safari ya kwenda Ivory Coast kushuhudia fainali hizo.

“Tunafuraha kuzindua promosheni ya 'Soka la Afrika Limeitika', inayowapa wateja wetu wapendwa fursa ya kipekee ya kuwa sehemu ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2024. Promosheni hii sio tu inaendana na dhamira yetu ya kutoa uzoefu usio na kifani bali pia inasherehekea ushiriki wa Tanzania katika fainali hizi kubwa Afrika," alisema Francis.