Wafugaji wakopeshwa vifaranga

28Nov 2023
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Wafugaji wakopeshwa vifaranga

ZAIDI ya wafugaji 30 mkoani hapa wamenufaika na Mradi wa Bulding for Better to Morrow (BBT) baada ya kukopeshwa vifaranga wa kuku 21,000 ili kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri katika sekta ya ufugaji.

Akizungumza jijini hapa wakati akigawa vifaranga 9,000 vyenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 56 kwa wafugaji hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya fedha ya EFTA, Nicomed Bohay, alisema hatua hiyo ni mkombozi kwa wanawake na vijana wanaojihusisha na sekta hiyo ya ufugaji.

“Fedha hizi ni pamoja na vifaranga, chakula, dawa na usafiri kwa wafugaji wetu ili tunapowakabidhi vifaranga wafuge bila kupata mawazo ya kutafuta chakula na dawa,” alisema.

Alisema kabla ya kukopeshwa vifaranga hivyo vinavyozalishwa na kampuni ya uzalishaji vifaranga bora ya Silverlands,  wafugaji hayo wamepata mafunzo ya ufugaji kwa siku saba.

“Hawa Silverlands wanaozalisha vifaranga pia wanatoa wataalamu wanaowasaidia wafugaji hawa kuwapa elimu na ushauri kila hatua ya ukuaji wa vifaranga lengo letu ni kuhakikisha mfugaji hapati hasara ili arudishe mkopo wake bila shida,” alisema.

Aliwaomba Watanzania kutumia fursa ya mkopo wa vifaranga wanaozalishwa na kampuni hiyo ili kuboresha maisha yao kwa kujiajiri na kujiingizia kipato cha kujikimu na mahitaji yao.

Alisema pamoja na mkopo wa vifaranga hao kwa wafugaji, wanatoa fedha        za kuwalisha hadi kuuzwa kama kuku wa nyama.

Aliwaomba wafugaji hao kufuga kwa kufuata ushauri na elimu waliyopatiwa ili warudishe mikopo yao na kuwezesha wafugaji wengine kukopeshwa.

Meneja Masoko wa Silverlands Tanzania, Mwanamvua Ngocho, aliwaomba wafugaji hao waliopata mkopo huo kwa awamu ya kwanza mkoani Arusha kuhakikisha wanafanya vizuri na kurejesha.

“Sisi Silverlands tunazalisha vifaranga bora, tunatoa mafunzo kituo chetu cha uzalishaji mkubwa wa vifaranga hawa kipo mkoani Iringa na tunatoa wataalamu wanaosimama na wafugaji hatua zote za ufugaji… tunaishukuru taasisi ya fedha ya EFTA kwa kufadhili mradi huu,” alisema.

Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Daniel Loiruck, aliwataka wafugaji hao kuzingatia mafunzo waliyopatiwa ili wawe wafugaji wakubwa wa kibiashara ndani na nje ya nchi.

Mnufaika wa mradi huo, Neema Rweyemamu, alisema amekopeshwa kuku 500 wakati akiwa amepatiwa mafunzo na Silverlands mkoani Iringa ya ufugaji wenye tija.