Wadaiwa kulima usiku kwa tochi ndani ya hifadhi ya Biharamulo

30Nov 2023
Daniel Limbe
BIHARAMULO
Nipashe
Wadaiwa kulima usiku kwa tochi ndani ya hifadhi ya Biharamulo

LICHA ya serikali kuweka mikakati madhubuti kudhibiti uharibifu wa misitu ya hifadhi nchini kwa lengo la kuepusha nchi kuwa jangwa siku za usoni, baadhi ya wakulima wameibuka na mbinu mpya ya kuingia kwenye hifadhi nyakati za usiku kufanya shughuli za kilimo kwa kutumia mwanga wa tochi.

Hatua hiyo inadaiwa kusababishwa na doria za mara kwa mara zinazofanywa na wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) kwenye msitu wa hifadhi ya Nyantakara na Biharamulo mkoani Kagera, kwa lengo kudhibiti uharibifu wa misitu nyakati za mchana,hivyo wananchi hao kulazimika kuingia usiku kutekeleza uharifu huo.

Meneja wa wakala wa huduma za misitu wilayani Biharamulo, Goodluck Malisa, ameiambia Nipashe Digital kuwa vitendo vya kuingia ndani ya misitu ya hifadhi usiku na kufanya shughuli za kibinadamu pasipo kibali cha mamlaka husika ni kosa kisheria, licha ya baadhi ya wananchi kuamua kuvunja sheria kwa makusudi.

Kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita wakala hiyo imefanya doria 64 kwenye msitu wa Nyantakara na Biharamulo katika eneo lenye ukubwa wa hekta 30,833 ambapo walikamata watuhumiwa 78, ng'ombe 1,071, majembe ya kulima kwa mkono 57, baiskeli 141, shoka 25, mapanga 45, mikuki 4, pikipiki 27, magunia ya mkaa 550, mbao 175 pamoja na kuteketeza matanuru ya mkaa 38.