- ni wa kupongezwa kwa hatua iliyofikiwa kwa kuanza kuzalisha sukari nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa Kamati hiyo, walipofanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi kinachomilikiwa kwa ubia baina ya NSSF na Jeshi la Magereza, mkoani Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Fatuma Toufiq amesema kuwa, wameridhishwa na uzalishaji wa kiwanda hicho na kuhimiza uzalishaji huo ufanyike kwa wingi ili kupunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge amesema Serikali imeonyesha nia ya kumaliza kabisa tatizo la sukari hapa nchini kwa kuhakikisha kiwanda hicho cha Mkulazi kinajengwa na kuongezwa nguvu katika uzalishaji wa sukari hapa nchini ambao wakati mwingine inalazimika kuagiza kutoka nje ili kukabiliana na mapungufu.
“Pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi lakini tayari tumeona nia ya serikali katika kupunguza tatizo la sukari hapa nchini kwani Kiwanda cha Mkulazi tayari kimekamilika kwa zaidia ya asilimi 95 na kimeanza uzalishaji wa sukari ambayo imeshaanza kuingia sokoni, tunapongeza sana Serikali” amesema Mwenyekiti huyo wa kamati ya Bunge.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema kuwa kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha tani elfu 50,000 kwa mwaka na uboreshaji utakavyofanyika utawezesha kiwanda hicho kuzalisha zaidi ya tani elfu 75,000.
“Serikali imeweka dhamira kuhakikisha nchi yetu sasa inaondokana na upungufu wa sukari, lengo letu kuongeza uzalishaji wa kutosha wa sukari kwenye viwanda vyetu vyote hapa nchini ikiwemo hiki cha Mkulazi ” amesema Naibu Waziri huyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hodhi ya Mkulazi, Dk Hildelitha Msita amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa wamejipanga kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kamati hiyo ili kuboresha mradi huo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba ameahidi kusimamia vizuri mradi huo ili uweze kuleta tija na kurudisha fedha za wanachama.
Mapema wiki iliyopita Kamati ya kudumu ya Bunge, Viwanda ,Biashara,Kilimo na Mifugo ilitembelea Kiwanda hicho ili kujiridhisha kusimama kwa uzalishaji wa sukari kutokana na mashamba ya miwa kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.









