TRA yafunga hoteli Singida

08May 2016
Elisante John
Singida
Nipashe Jumapili
TRA yafunga hoteli Singida

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) imeifunga hoteli maarufu ya Country Inn and Suites ya mjini Singida, kutokana na deni linalofikia Sh. Milioni 32 la kodi ya mapato, ongezeko la thamani na tozo ya ufundi stadi (SDL).

hoteli ya Country Inn and Suites.

Zoezi la kuifunga hoteli hiyo iliyopo mtaa wa Bomani, pembezoni mwa ziwa Singidani, lilitekelezwa na kampuni ya udalali ya Mchinga Auction Mart ya Dodoma, chini ya usimamizi wa jeshi la polisi.

Mkurugenzi wa Mchinga, Enock Lukumbo alisema kampuni yake imelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupokea maelekezo kutoka TRA juu ya deni hilo.

Alisema mmiliki wake alipewa notisi ya kulipa tangu Desemba, mwaka jana.

“Hoteli hii tumeikamata na tumeifunga kwa maelekezo tuliyopewa na TRA, utaratibu baada ya hapa zitapita siku 14 kama hajalipa basi tutapeleka ripoti TRA ambao watatupa kibali kutangaza kwenye gazeti, kisha kuandaa mnada wa kuiuza kulipia deni analodaiwa,”alifafanua Lukumbo.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Singida, John Msangi alisema ingawa mamlaka hiyo ilijaribu kutumia ushawishi mkubwa tangu mwaka 2005 ili mteja huyo alipe deni hilo, alishindwa kuonyesha ushirikiano.

Msangi alisema TRA ilimwita mteja huyo ofisini wakakubaliana amalize deni kwa awamu nne tangu Desemba mwaka jana.

"Lakini hata hivyo alishindwa kuonyesha ushirikiano baada ya kulipa Sh. 600,000 na tangu hapo hajaonekana na kila anapopigiwa simu wala hapokei," alisema Meneja huyo wa mkoa.

Alisema pamoja na juhudi za TRA kukamata akaunti za hoteli hiyo zilizopo benki ya CRDB na NBC, hawakuambulia kitu kutokana na kutokuwako na fedha kwa ajili ya kulipia deni hilo.

Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani, Nestory Bukha aliyeshuhudia zoezi hilo, aliwataka wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao katika eneo la mtaa wake na wengine hapa nchini, kuhakikisha wanalipa kodi TRA, ili kuipa serikali uwezo wa kuhudumia jamii.

Wafanyakazi wa hoteli hiyo akiwemo msimamizi mkuu, Samwel Luhende, wakizungumza baada ya eneo lao la kazi kufungwa walisema hatua hiyo itaathiri maisha yao kwani kuna madai ya mishahara inayoanzia mwezi mmoja hadi minne.