Shule ya Sekondari Jakaya Mrisho Kikwete yaunganishiwa umeme wa jua

26Feb 2024
Julieth Mkireri
CHALINZE
Nipashe
Shule ya Sekondari Jakaya Mrisho Kikwete yaunganishiwa umeme wa jua

KAMPUNI ya Matheotechs imeunganisha umeme wa jua katika shule ya Sekondari ya Jakaya Mrisho Kikwete iliyopo katika Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, utakaowasaidia wanafunzi kuweza kusoma muda wote watakaokuwa shuleni hapo.

Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni hiyo Theobald Bonaventure amesema wamejitolea msaada huo kuunga mkono jitihada za Rais katika Uwekezaji kwenye shule.

Bonaventure pia amesema kuunganisha umeme huo katika shule ya Jakaya ni pamoja na kulinda hadhi ya jina la Rais Mstaafu sambamba na kupunguza gharama za umeme wa Tanesco.

"Kila mwaka tumekuwa tukirudisha kwa jamii kile tunachopata na tunaendelea kufanya hivyo tumefunga umeme huu zaidi pia tukilenga kuwa na ufaulu mkubwa kwa wanafunzi ambao watapata muda wa kujisomea wakati wote" amesema.

Mradi huo umegharimu sh. milioni 16 na utaunganishwa katika vyumba vya madarasa vya shule hiyo.

Akizindua mradi huo Mbunge wa Chalinze, Ramadhani Kikwete ameishukuru Kampuni hiyo kwa kusaidia uwepo wa umeme wa jua katika shule hiyo ambao utawezesha wanafunzi kujisomea muda wote bila kukatika.