Kicheko chatawala Ngorongoro watalii, mapato yakiongezeka

27Feb 2024
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kicheko chatawala Ngorongoro watalii, mapato yakiongezeka

​​​​​​​IDADI ya watalii wanaotembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imeongezeka sambamba na mapato yatokanayo na wageni hao.

Imebainishwa na uongozi wa mamlaka hiyo uliojawa tabasamu kwamba, kwa mwaka 2022/23, idadi ya wageni wanaotembelea NCAA ilikuwa 752,232 kulinganishwa na wageni 191,614 waliotembelea hifadhi hiyo mwaka 2020/21.

Kamshina Mkuu wa NCAA, Richard Kiza amebainisha hayo alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ambayo mamlaka hiyo imepata katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kamishna Kiza alisema hayo ni miongoni mwa mafanikio ambayo mamlaka hiyo imepata kwa kipindi hicho, ikisifu jitihada zilizofanywa na Rais Samia kuinua sekta ya utalii na uhifadhi tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.

Amesema NCAA inatarajia kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni moja katika mwaka huu wa fedha (2023/24) na kuiongezea serikali mapato.

Tangu Julai 2020, mapato ya utalii nchini yanakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo kupelekwa hazina. Awali yalikusanywa na mamlaka za uhifadhi; Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), NCAA na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA).

Kamishna Kiza amesema kutokana na jitihada za serikali chini ya Rais Samia, NCAA sasa inapata fedha kwa wakati na kufanya ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa kwa wageni.

Amesema kutokana na ongezeko hilo la watalii, ukusanyaji wa mapato, unatarajia kuongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 200 kwa mwaka huu wa fedha.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, mamlaka hiyo imepata mafanikio makubwa katika shughuli zake za kila siku.

Amesema kuwa Rais Samia amekuwa chachu ya maendeleo ya mamlaka hiyo kutokana na kushiriki kwake katika filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza idadi ya watalii wanaofika kutembelea hifadhi.

"Juhudi za Rais Samia katika kukuza utalii hazikuishia tu kwenye filamu ya Tanzania The Royal Tour bali pia katika kuhakikisha mamlaka inapata fedha za uendeshaji kwa wakati, jambo ambalo limesaidia kulipa mishahara pamoja na stahiki nyingine za watumishi kwa wakati, kujenga miundombinu ya ofisi, barabara, maji na umeme na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kuona huduma zinazotolewa kwa watalii zinakuwa za kisasa na zisizo na usumbufu," amesema.

Kamishna Kiza amesema kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani Machi 19, 2021, alikuta sekta ya utalii ikiwa na hali mbaya kiasi kwamba idadi ya wageni ilishuka, lakini kutokana na maono yake  na juhudi zake binafsi katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali yake, mamlaka imeshuhudia mambo makubwa.

Amesema katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023/24, hifadhi hiyo imepokea wageni 534,065, likiwa ni ongezeko la asilimia 10 kulinganishwa na idadi ya wageni waliotembelea hifadhi katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23.

Kuhusu mapato yatokanayo na utalii, Kamishna Kiza amesema yameongezeka kutoka Sh. bilioni 31 mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh. bilioni 171 mwaka

2022/23.

"Hiki ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kukusanywa na mamlaka. Mapato yanatarajiwa kuongezeka zaidi na kufikia takribani Sh. bilioni 200 kwa mwaka kwani katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2023/24, Sh. bilioni 123 zimekusanywa.

"Mapato haya yameongezeka kwa asilimia 13 kulinganisha na mapato yaliyokusanywa katika kipindi hicho hicho mwaka 2022/23," amebainisha.

Kamishna huyo wa uhifadhi pia amesema kuwa mbali na kutangaza Tanzania kupitia filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour, Rais aliagiza NCAA ipatiwe fedha za mkopo wa kukabiliana na athari za UVIKO-19 Sh. bilioni 6.645 ambazo zilitumika kuimarisha miundombinu ya barabara na kununua mitambo pamoja magari makubwa ya kutengenezea barabara.

Amesema kuwa fedha hizo pia zilitumika kuimarisha viwanja vya ndege pamoja na miundombinu mingine ya utalii ili wageni wavifikie vivutio vya utalii kwa urahisi.

Amesema serikali pia imetenga Sh. bilioni 69 kwa ajili ya kujenga tabaka gumu kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 29.5 kutoka lango kuu la kuingilia NCAA hadi Seneto.

Amesema Novemba mwaka 2022, Rais Samia alifanya ziara ya kikazi China na kupata Sh. bilioni 25 kwa ajili ya kuendeleza Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark pamoja na miundombinu mingine ya utalii ikiwamo nyumba ya makumbusho itakayojengwa katika lango kuu la kuingilia Ngorongoro.

Kamishna Kiza ametaja mafanikio mengine waliyopata katika miaka mitatu ya Rais Samia madarakani yanajumuisha kudhibiti ujangili wa tembo kwa kuimarisha ulinzi ndani na nje ya hifadhi, huku wakishuhudia ongezeko la faru kwa asilimia 25. NCAA inamiliki asilimia 25 ya faru weusi waliopo nchini.

Kiongozi huyo wa NCAA pia ametoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa serikali kuhamisha wananchi na mifugo ndani ya hifadhi hiyo, akieleza madhara ya kiikolojia ya ongezeko la watu na mifugo hifadhini.

Amesema kuwa wakati NCAA inaanzishwa mwaka 1959, kulikuwa na wananchi wasiozidi 8,000. Kati yao, 4,000 ni waliokuwa Ngorongoro na 4,000 waliohamia kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Amesema kuwa kipindi hicho idadi ya mifugo ya wananchi wakati huo ilikuwa takribani 261,000.

Hali hiyo ni tofauti na miaka ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini (NBS), wananchi katika Tarafa ya Ngorongoro wameongezeka kutoka 8,000 mwaka 1959 hadi kufikia zaidi ya watu 100,000 na mifugo ikiongezeka kufikia zaidi ya 850,000 (Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022). Eneo hilo lina ukubwa wa kilomita za mraba 8,292.

KUHUSU NCAA

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ilianzishwa kwa Sheria Na. 413 ya Mwaka 1959 kwa kuigawa Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA), ili kuanzisha hifadhi yenye upekee duniani; ina wanyamapori, mifugo na binadamu.

Kamishna Kiza ameyataja mambo yaliyosababisha hifadhi hiyo kugawanywa kuwa ni kuendeleza uhifadhi wa maliasili na malikale, kusimamia maendeleo ya jamii ya watu wanaoishi ndani ya mamlaka Wahdzabe, Masai, Datoga na kuendeleza utalii.